Stars mguu sawa kuivaa Niger, Samatta afunguka
Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’
Mbwana Ally Samatta amesema wamejipanga kupambana na kuanza vyema Kampeni za
kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za AFCON 2023 zitazofanyika nchini Ivory
Coast.
Taifa Stars itaanza Kampeni hiyo kesho Jumamosi (Juni 04), kwa
kucheza ugenini dhidi ya Niger nchini Benin, na tayari imewashawasili Cotonou
kwa ajili ya mchezo huo, utakaoanza majira ya saa moja kwa saa za Afrika
Mashariki.
Samatta amesema dhamira kubwa waliyoondoka nayo jijini Dar es
salaam jana Alhamis ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo wakiamini
kufanya hivyo itawawezesha kuwa na mwanzo mzuri wa safari yao ya kucheza AFCON
2023.
“Mawazo yetu ni kuanza vizuri kampeni za AFCON 2023, kwa sababu
ndio mchezo wetu wa kwanza, bahati mbaya tunaanzia ugenini, lakini upande
mwingine ni bahati nzuri kwa sababu unapopata matokeo mazuri ugenini kwa kiasi
fulani inakuongezea kujiamini katika kamepni nzima, kwa hiyo lengo ni kwenda
kuanza vizuri.”
“Tunaamini mipango na mikakati yetu itatimia kwa sababu
tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wetu wa kesho dhidi ya Niger, niwaombe
watanzania kuwa kitu kimoja na kuiombea timu yao ili iweze kufanikiwa kupata
ushindi kesho na kufanikiwa kupata tiketi ya kucheza AFCON 2023.”
“Tunafahamu Niger nao wanatamani kwenda kushiriki Fainali za
AFCON mwakani, sisi pia tunatamani kurudi tena baada ya kushiriki miaka miwili
iliyopita, kwa hiyo lazima mchezo utakua mgumu, kwa sababu kila timu inaamini
kwamba kuanza vizuri katika mchezo wa kwanza maana yake unapata nafasi ya kuwa
na Kampeni nzuri” amesema Samatta.
Baada ya mchezo wa kesho Jumamosi (Juni 04), Stars itarejea
jijini Dar es salaam kucheza mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi F dhidi ya
Algeria utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 08.
No comments
Post a Comment