Simon Msuva: Tuna kumbukumbu nzuri hapa Benin
Kiungo Mshambuliaji Simon Msuva amewataka Watanzania kuwa na
imani kubwa na timu yao ‘Taifa Stars’ kuelekea mchezo wa Kwanza wa kuwania
kufuzu Fainali za Afrika ‘AFCON 2023’ dhidi ya Niger.
Taifa Stars imewasili nchini Benin tayari kwa mchezo huo
utakaopigwa kesho Jumamosi Juni 04 2022 katika Uwanja wa taifa wa nchi hiyo
(Stade de l’Amitie) ambao unatumiwa na timu ya taifa ya Niger kama uwanja wake
wa nyumbani kufuatia Uwanja wa taifa wa nchi hiyo (Stade Seyni Kountché)
kushindwa kufikia vigezo vya CAF.
Msuva amesema wachezaji wote wa Stars baada ya kuwasili Benin
wapo katika hali nzuri na wana morari kubwa ya kupambana, hivyo amewataka
Watanzania kuzidi kuwaombea, ili wafanikishe lengo la kuondoka ugenini na alama
tatu.
“Tuna Morari ya hali ya juu kama wachezaji, tunamshukuru mungu
wachezaji wote ni wazima, hapa tulipokuja tumekuja kwa mara ya pili, kama
mnakumbuka mara ya kwanza tulipata matokeo dhidi ya wenyeji halisi Benin kama
mnakumbuka, ninaamini kesho tutakua na kumbukumbu ya ushindi tulioupata hapa,
japo tutacheza na timu tofauti.”
“Wachezaji wanafahamu umuhimu wa huu mchezo, kwa sababu ndio
mchezo wetu wa kwanza na inatulazimu kupambana ili tupate ushindi ambao
utatusaidia katika kampeni yetu ya kuwania kufuzu AFCON 2023, tunawaomba
watanzania watuombee ili tuweze kupambana na kupata matokeo mazuri tukiwa hapa
ugenini.” amesema Msuva
Baada ya mchezo wa kesho Jumamosi Stars itarejea jijini Dar es
salaam kucheza mchezo wa Mzunguko wa Pili wa Kundi F dhidi ya Algeria
utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 08 2022.
No comments
Post a Comment