Wanawake wa  Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania mkoani Njombe, wameagizwa kuacha kupanga safu ya uongozi badala yake watende haki katika chaguzi za ndani zinazoendelea nchini na katika mkoa huo.

Agizo hilo lometolewa na Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Njombe Scolastika Kevela, alipokutana na viongozi wa jumuiya hiyo katika ziara yake aliyoifanya katika wilaya ya Ludewa ili kutoa maelekezo mbali mbali juu ya Chama na Jumuiya.

“Katika chaguzi tunazoendelea nazo,tuache kupanga safu kwasababu ukiona mtu anafanya hivyo maana yake mtu huyo hajiamini na kwa muda wote hajafanya kazi akisubiri nyakati za uchaguzi,kiongozi wa namna hiyo ni kumpiga chini”amesema Scolastika Kevela

Aidha Bi,Kevela ametoa wito kwa wananchi na wanawake wa mkoa huo kuendelea kulea familia kwa bidii ili kuondokana na tatizo la utapiamlo kwa kuwa mkoa huo upo imara kiuchumi.

“Tukalee familia zetu kwa bidii ili tuondokane na mdudu anayeitwa utapiamlo na kama sio wewe basi ukimwona jilani yako mwambie”alisema Bi,Kevela

Baadhi ya wanawake akiwemo Ester Mwalongo na Reinihada Tweve wamekiri kuwa nyuma katika maswala ya malezi kwa watoto na kusababisha utapiamlo kutokana na kuwa bize katika kazi huku wakiwa na uchumi mzuri.