Tukio la uvamizi wa mwanamke Kenya:mmoja ashikwa akitoa pesa kwenye simu ya muathiriwa

Mtuhumiwa mmoja wa
uvamizi uliotekelezwa na genge la majambazi kwa mwanamke mmoja mtaani Rongai
nchini Kenya, amekamatwa na maafisa wa polisi akitoa kiasi kikubwa cha pesa
kwenye duka la kutolea pesa
Mwanamume huyo ambaye
sasa anawasaidia polisi katika msako wa kuwakamata wenzake, alikamatwa Jumatatu
mtaani Mwiki, Kasarani akitoa shilingi 240,000 za Kenya kutoka duka la Mpesa.
Mtuhumiwa huyo anaaminika
kuwa mwanachama wa genge la wezi ambao walikuwa wamejihami kwa bunduki na
kumwibia mwanamke huyo mkoba wake, simu na vitu vingine vya bei ghali pamoja na
kumshurutisha kuwapa nambari yake ya siri (PIN) ya Mpesa.
Mhudumu wa duka la Mpesa
ambako pesa hizo zilitolewa pia alikamatwa na maafisa wa polisi ili kusaidia
katika uchunguzi.
“Kufikia sasa tumekamata
washukiwa wawili. Tunaendelea kuwahoji ili kupata taarifa zaidi,” afisa huyo
amenukuliwa akisema.
“Ripoti za awali zinaonyesha
kuwa kikosi cha majambazi ambacho kilimvamia mwanamke huyo kiliongozwa na afisa
wa polisi wa zamani,” alisema.
Waziri wa Usalama wa
Kenya Fred Matiang’i alitembelea eneo la tukio akiwa ameambatana na Inspekta
Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai na Mkuu wa Kitengo cha Huduma Spesheli
katika Idara ya Upepelezi wa Jinai (DCI) Pius Gitari na kuwahakikishia wakazi
kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa.
Ziara ya watatu hao pia
ilidhamiria kufahamu hali halisi ya usalama eneo hilo, kukiwa na malalamishi ya
wakaazi ambao wamelalamika kudorora kwa usalama na kuhimiza polisi kuchukua
hatua.
No comments
Post a Comment