Idadi ya vifo yafikia 79, Rais atangaza maombolezo
Serikali nchini Burkina
Faso, imesema idadi ya watu waliouawa katika shambulio lililofanywa na kundi
linaloshukiwa kuwa ni la wanajihadi wenye msimamo mkali walio na uhusiano na
Islamic state mjini Seytenga Jimbo la Sahel kaskazini mwa Burkina Faso, imefikia
79.
Kufuatia vifo hivyo, Rais
wa mpito wa Burkina Faso, Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, ametangaza
kipindi cha saa 72 cha maombolezo ya kitaifa, ikiwa ni muda mfupi baada ya
kupatikana kwa miili mipya 29.
Kulingana na agizo la
Rais, maombolezo hayo ya kitaifa yameanza hii leo Juni 14, 2022 na yatamalizika
siku ya alhamisi Juni 16, 2022 huku Umoja wa Ulaya (EU), ukilaani shambulio
hilo na kusema idadi hiyo ya waliouawa inaweza kufikia watu 100.
“Maombolezo haya
yatazingatiwa katika eneo lote la kitaifa, kwa kumbukumbu ya waathirika wa
shambulio lililofanywa na watu wasiojulikana wenye silaha dhidi ya mji wa
Seytenga, katika mkoa wa Séno, mkoa wa Sahel, wakati wa usiku wa Juni 11 hadi
12,” amesema Luten Dabima.
“Na katika kipindi hiki,
bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kwenye majengo yote ya umma na katika
uwakilishi wa Burkina Faso nje ya nchi mambo ya sherehe maarufu na hafla za
kiburudani ni marufuku hadi tutakapomaliza maombolezo,” amesisitiza Rais huyo
wa mpito.
Naye Mkuu wa Diplomasia
ya Ulaya Josep Borrell amesema mchakato uliotumiwa na kundi la kigaidi
lililofanya shambulio hilo, kwa kunyonga kila mtu katika kijiji hicho ni wa
kutisha na unapaswa kulaaniwa vikali na Mataifa yote.
Licha Luteni Kanali
Damiba kuingia madarakani kwa kumpindua Rais Roch Marc Christian Kaboré, ambaye
alishutumiwa kwa kutofanya kazi dhidi ya ukosefu wa usalama, mashambulizi ya
vuguvugu hizi zenye mafungamano na al-Qaeda na Dola ya Kiislamu bado yamekwama.
Taarifa zinasema kuwa kwa
kipindi cha miezi mitatu karibu raia zaidi ya 300 wameuawa wakiwemo na
wanajeshi katika eneo hilo la kaskazini na mashariki mwa nchi ya Burkina Faso
linayopakana na nchi ya Mali na Niger.
Tangu mwaka wa 2015,
mashambulizi yanayohusishwa na wanajihadi yameua zaidi ya watu 2,000 na watu
zaidi ya milioni mbili kukimbia nchini Burkina Faso.

No comments
Post a Comment