Jemedari Said amrudisha darasani Haji Manara
Saa 24 baada ya Msemaji wa klabu ya Young Africans Haji Sunday
Ramadhan Manara kuweka wazi namna anavyochukizwa na dhihaka anazozipata kutoka
kwa baadhi ya watu nchini Tanzania kwa kigezo cha ulemavu wake wa ngozi,
Mchambuzi wa Michezo Jemedari Said Kazumari amempa somo kwa kumtaka aache
kuwadhihaki wengine.
Jemedari ambaye kwa sasa hana maelewano na Haji Manara ametumia
Kurasa zake za Mitandao ya Kijamii kumfikishia ujumbe huo hasimu wake, huku
akianza na maneno mazuri ya kuunga mkono kauli ya Manara kupinga dhihaka dhidi
ya watu walemavu.
Jemedari ameandika: WATANZANIA TUBADILIKE, HII SIO SAWA..!
Ukimsikiliza Afisa Mhamasishaji wa Yanga utaona namna gani
anaumizwa na dhihaka anayofanyiwa na Watanzania wenzake ambayo hajawahi
kufanyiwa akiwa nje ya Nchi yake pendwa aliyozaliwa na kuipenda.
Kama kuna Watanzania wanamfanyia dhihaka hii bila sababu yoyote,
yani anapita tu mtaani unamdhihaki kwa ulemavu wake wanakosea sana sana sana.
Hatupaswi kufanya namna hiyo kwani jamii na familia zetu
zinatufundisha kuwa na huruma na watu wenye mapungufu ya kimaumbile kwa namna
yoyote ile.
Watanzania wanapaswa kufuata mafundisho mema ya Dini zetu Kuu 2
ambazo zote zinapinga hili kama zinavyopinga mambo mengi maovu yasiyo na maana.
Ulemavu haupaswi kuwa kinga kwa mmoja wetu kufanya dhihaka kwa
wengine kisa yeye mlemavu, akidhihakiwa yeye kwa ulemavu wake ama namna
nyingine yoyote, aanze kusaka huruma ya jamii.
Afisa mhamasishaji amedhihaki wangapi kwa maumbile yao?
Alimdhihaki Makamu Mwenyekiti wa Yanga na kumuita Kilo 800 tena mbele ya Camera
za Waandishi Habari, huko alikotembea mwenzetu ile ni sawasawa tu.
Afisa mhamasishaji amemdhihaki mara ngapi mwekezaji wa Simba kwa
Uhindi wake? Vipi huko Duniani wanakoenda wenzetu hii haina shida? Wangapi
wamedhihakiwa na kuitwa majina yasiyofaa iwe dhahiri au kwa kificho na Bwana
huyu ambaye analalamika yeye kudhikiwa?
Ukidhihaki wenzio kwa unayoyaona yanafaa kwako, usiwachagulie
wewe wakudhihaki kwa lipi. Dawa ni kutowadhihaki ili nawe wakulindie udhaifu
wako.
Vingenevyo kuwa mvumilivu tu bro, kuna walemavu wa ngozi
wanapaswa kulalamikia hilo lakini sio wewe au wale wenye tabia kama zako, kwani
unaowadhihaki ni Binadamu kama wewe wana wazazi, mioyo, ndugu na familia kama
wewe. Wanaumizwa na dhihaka zako ila wanavumilia wao na familia zao, nawe
vumilia tu usitangulize ulemavu wako
Mwalimu wa Madrasa anaejua Dini vilivyo hawezi kuwa wa mwanzo
kutakia wengine mabaya tena hadharani na kushinda kwenye vilabu vya pombe
analewa halafu analalamika jamii yake kukosa Dini. Nani anapaswa kuwa mfano
sasa kama sio wanazuoni wa mambo ya Dini?
NB: Ukiishi kwenye nyumba ya vioo usiwe wa kwanza kuanzisha
ugomvi wa mawe, wajuba watakupopoa tu bila kujali mambo mengine.

No comments
Post a Comment