Aden Rage aupongeza Uongozi Simba SC
Aliyekua Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC, Ismail Aden Rage
ameupongeza Uongozi wa sasa wa klabu hiyo kwa dhamira yao ya kutaka kuuendeleza
Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo eneo la Bunju jijini Dar es salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez alikaririwa na vyombo
vya habari akisema wapo katika katika mpango mkakati wa kuendeleza ujenzi wa
Uwanja wa Mo Simba Arena, na pesa zitakazopatikana kwenye Kampeni ya ‘Nani
Zaidi’ zitatumikwa kwenye ujenzi huo.
Rage amesema, hana budi kuupongeza Uongozi wa Simba SC kwa
juhudi walizozionesha hadi kufikia hatua ya timu ya klabu hiyo kuwa na eneo la
kufanyia mazoezi.
Amesema ni hatua kubwa kwa klabu kama ya Simba SC kuwa na Uwanja
wake wa Mazoezi, tofauti na wakati akiwa madarakani, ambapo walitumia viwanja
vya kukodi kwa gharama kubwa kwa kila siku.
“Niwapongeze viongozi wa
Simba SC kwa juhudi za kuhakikisha timu yetu imekua na eneo la kufanyia
mazoezi, wakati mimi nipo madarakani eneo la Bunju lilikuwa pori na halikua na
kitu chochote, lakini kwa msaada wa wanachama na Uongozi leo kuna jambo
limefanyika.”
“Niwaombe viongozi wangu, wahakikishea wanatumia mapesa
wanayoyapata kwa mwaka mzima kuendeleza kile kiwanja kwa sababu kwa sasa
tunatumia gharama kubwa kwa kuiweka kambini timu yetu, ninaamini kama haya
wanayoyafanya sasa watayafanikisha Simba SC itakua mbali na itapiga hatua
kubwa” amesema Rage.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzalez alitembelea
eneo la Uwanja wa Mo Simba Arena lililopo Bunju jijini Dar es salaam,
akiongozana na msanifu majengo (architect).
Barbara alisema, zoezi la kujenga majukwaa na miundo mbinu
mingine ya Uwanja wa Mo Simba Arena wamelidhamria na zimebaki siku chache kabla
ya Bodi ya Wakurugenzi itakayokutana Ijumaa (Juni 17) ili kumpitisha
mkandarasi.

No comments
Post a Comment