Wakurugenzi na wakuu wa idara kuanza kupimwa katika utendaji wao
Serikali inakusudia kupima utendaji wa
Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kutumia viashiria muhimu hususan usimamizi
wa mapato na makusanyo ya ndani pamoja na upelekaji wa fedha kwenye
miradi ya maendeleo.
Tamko hilo limetolewa na Waziri mkuu Kassim
Majaliwa wakati akitoa Hoja ya
Kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Bungeni jijini Dodoma. Amesema hatua hiyo ni katika kuhakikisha dhamira nzuri
ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inayojiakisi kwenye Mpango na Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2022/2023 inafikiwa.
Mhe. Majaliwa amesema watendaji hao pia
watapimwa kwa namna wanavyosimamia mikopo ya asilimia 10 ikiwa ni
pamoja na marejesho, usimamizi wa miradi ya maendeleo na uzuiaji na utekelezaji
wa hoja za ukaguzi zinazoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG).
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali
imejipanga vema kuendelea kusimamia suala la uwajibikaji katika utumishi wa
umma kwa kuweka mikakati mbalimbali. “Mikakati ipo katika kuimarisha
uwajibikaji hususan kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni pamoja na
kupima utendaji wa utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara.”
Amesema mkakati mwingine ni
kongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa
Mikoa na Wilaya kutoka shilingi bilioni
57.44 hadi shilingi bilioni 79.09 ili kuwezesha utekelezaji wa
majukumu ya ofisi hizo.
“Sambamba na ongezeko hilo la Bajeti katika
mwaka 2022/2023, Serikali pia, imehuisha muundo wa Sekretarieti za Mikoa
kwa kuboresha iliyokuwa Sehemu ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa na
kuwa Sehemu ya Menejimenti, Ufuatiliaji na Ukaguzi ili
kuimarisha ufuatiliaji wa mapato, matumizi na utekelezaji wa miradi katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa.”
Amesema Serikali itaendelea kuwajengea uwezo
Madiwani, Mafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kupitia Programu ya
Uimarishaji Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la
kuongeza uelewa wa majukumu yao kisheria, kuimarisha mahusiano
yao na viongozi wa kisiasa na kusimamia ipasavyo miradi ya
maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao pamoja
na ukusanyaji wa mapato.
Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea
kujenga mifumo na miundo wezeshi katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili
kuboresha utendaji kazi unaojali matokeo. “Eneo hili linahitaji uwepo wa
mifumo na miundo imara ambayo itawezesha kujenga msingi thabiti wa usimamizi wa
utendaji kazi wa Serikali.”
Amesema hatua hizo zinajumuisha kupitia upya
miundo na majukumu ya Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali,
Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika
eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuziimarisha pamoja na kujenga uwezo wa
watumishi katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema
Serikali imeanza maandalizi ya Sera ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa kuzihusisha
taasisi simamizi zinazohusika na ufuatiliaji na tathmini ili kuchambua maeneo
wanayosimamia na kuhakikisha maeneo yote muhimu yanajumuishwa ikiwemo usimamizi
wa mipango ya maendeleo na utendaji wa Serikali kwa ujumla.
“Sambamba na hatua hizo, tayari, Serikali
imekamilisha Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo ambao utaanza
kutumika Julai, 2022. Mfumo huo, pamoja na mambo mengine utasaidia Serikali
kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na
hivyo kuongeza tija na thamani ya matumizi ya fedha za umma kwenye miradi
husika.”
Vilevile, Waziri Mkuu amesema Serikali
imehuisha Muundo na Mgawanyo wa Majukumu wa Ofisi ya Waziri Mkuu hususan
kwa upande wa Sera, Uratibu na Bunge ili kuimarisha jukumu la ufuatiliaji na
tathmini. “Lengo ni kuhakikisha taarifa za ufuatiliaji na tathmini kutoka
katika wizara na taasisi za Serikali zinafanyiwa uchambuzi wa kina pamoja na
kutoa mrejesho kuhusu utendaji wa Serikali.”
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya
Fedha na Mipango kufanyia kazi changamoto ya uhaba wa wataalamu wa ufuatiliaji
na tathmini; kazi za tathmini kufanyika kwa ufanisi na uwepo wa mifumo mingi ya
ukusanyaji wa taarifa yenye kuathiri ubora wa takwimu.
Amesema Serikali itaendelea kufanya tathmini
ya ujuzi unaohitajika, kufanya tathmini ya mifumo ya ufuatiliaji na tathmini
iliyopo kwenye taasisi za Serikali, kuandaa Kanzi-Data ya Watumishi wenye
utaalamu wa masuala ya ufuatiliaji na tathmini, kuongeza matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye ufuatiliaji na tathmini na kuimarisha
vitengo vya ufuatiliaji na tathmini ili kujenga mfumo jumuishi wa ufuatiliaji
na tathmini ambao utawezesha kufuatilia, kuchambua na kupata taarifa halisi na
kwa wakati za utendaji wa Serikali.
No comments
Post a Comment