Walioathiriwa na tembo Nachingwea watakiwa kujiorodhesha ili wafutwe machozi
Wakulima ambao mashamba yao yalivamiwa na kuharibiwa
mazao yao ya kilimo na tembo wameombwa wajiorodheshe ili wapate kifuta machozi.
Wito huo ulitolewa na mkuu wa idara ya
maliasili wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Lington Nzunda katika kijiji
cha Kitandi wilayani Nachingwea, mkoa wa Lindi wakati akizungumza na wananchi
kupitia mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho.
Nzunda alisema wakulima wote ambao
mazao yao yameharibiwa na kuliwa na ndovu hawanabudi kujiorodhesha ili walipwe
kifuta machozi( fidia). Kwani ni dhamira ya serikali kuona wakulima hao
wanapata kifuta machozi.
Aliwaasa wakulima wa kijiji hicho na
wengine waliopo wilayani Nachingwea ambao mshamba yao yameharibiwa na
tembo wakamilishe zoezi hilo haraka kabla ya tarehe 31.06.2022.
"Jiorodhesheni ili majina yenu
yafikishwe kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya yaweze kupelekwa
Dodoma. Msije kulalamika na kulaumu baadae kama hamtajiandikisha," Nzunda
alisisitiza na kuonya.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya
Nachingwea, Hashim Komba aliwaasa wakulima wilayani humo wazingatie na kufanyia
kazi maelekezo ya maofisa wanyama pori juu ya kujilinda na kulinda mashamba yao
dhidi ya tembo.
Alisema kama watazingatia na kufanyia
kazi maelekezo ya maofisa wanyama pori wataweza kujilinda na kulinda mashamba
yao kuharibiwa. Ikiwemo kupanda pilipili kuzunguka mashamba yao.
Hivi karibuni maofisa na askari wa
mamlaka ya usimamizi wanyamapori nchini(TAWA) wamekuwa wakitoa elimu ya jinsi
ya kujilinda na kulinda mashamba dhidi ya tembo katika maeneo mbalimbali nchini
ikiwamo katika wilaya ya Nachingwea.
No comments
Post a Comment