Askari uhifadhi watakiwa kujenga uhusiano mzuri na wananchi
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amewataka askari wa uhifadhi nchini
kujenga mahusiano mazuri na jamii inayozunguka maeneo ya hifadhi wanazozisimamia
kwa kufanya kazi kwa kushirikiana nao katika masuala mbalimbali.
Ameyasema
hayo Mkoani Kilimanjaro katika ziara ya kikazi alipotembelea Shamba la Miti la
West Kilimanjaro kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu na kusikiliza
changamoto zinazowakabili Askari Uhifadhi kwa ili kuzipatia ufumbuzi.
“Jamii
ikiwa haina mahusiano mazuri hata ninyi haya mashamba hamuwezi kuyaendeleza
vizuri, kwa hiyo lazima muhakikishe mnajenga mahusiano mazuri,” Masanja
amesisitiza.
Amesema
kuwa jamii inapokuwa hairidhishwi na utendaji kazi wa wahifadhi kunakuwa na
migongano kati ya wananchi na wahifadhi hao na kupelekea wahifadhi kuchukiwa na
wananchi.
Masanja
amewapongeza Askari Uhifadhi wa Shamba la Miti la West Kilimanjaro kwa
kuendeleza mahusiano mazuri na jamii kwa kugawa miche, kutoa ajira na kugawa
magogo ya kutengeneza samani.
Kuhusu
changamoto ya moto katika mashamba, Masanja ameelekeza wahifadhi kwenye
mashamba yote nchini kushirikiana na Serikali za Mitaaa ili wananchi wanapoanza
kuandaa mashamba yao wapate taarifa mapema na kuwaelekeza namna bora ya
kudhibiti moto kwa lengo la kuukinga usisambae kuepuka hasara inayotokana na
moto.
Aidha,
amewataka wahifadhi wanaozunguka mlima Kilimanjaro kupanda miti kuzunguka mlima
huo na kuhakikisha wanagawa miche ya miti kwa wananchi ili kuuzuia mlima
usiendelee kuyeyuka.
Kwa
upande wake Mhifadhi Mkuu Shamba la Miti West Kilimanjaro, Masawanga Ismail
amesema kuwa shamba limeendelea kuwa na uhusiano mzuri na vijiji na taasisi
zinazolizunguka ambapo imekuwa msaada mkubwa hasa wakati wa matukio ya moto,
upandaji wa miti na uhalifu ndani ya msitu.
Ameongeza
kuwa shamba limekuwa likitoa mashamba ya kulima mazao ya chakula kwa jamii
katika maeneo yanayovunwa miti kwa ajili ya maandalizi ya mashamba mapya ambapo
kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 limetoa ploti zisizopungua 640.
Pia,
amesema shamba limekuwa likitoa misaada mbalimbali kwa jamii inayolizunguka
kama usafiri kwa wagonjwa, wafiwa na taasisi mbalimbali na kugawa miche ya miti
takribani laki moja na elfu kumi na tano katika mwaka wa fedha 2021/2022 na
kutoa elimu ya ufugaji nyuki kwa vikundi vitano ambavyo vina wajumbe 95 vyenye
jumla ya mizinga 250 ambavyo kwa mwaka huu vimezalisha asali kilo 200.
Kuhusu
suala la utalii, Ismail amesema kuwa shamba hilo kwa mwaka huu limepokea
watalii elfu 40 ambao wameingizia Serikali Dola za Kimarekani 70,335 na fedha
za kitanzania takriban milioni 103.6.
Amesema
mapato hayo yanatokana na vivutio vya utalii vilivyomo kwenye shamba hilo kama
mapango ya Grumeti na Mikingamo, Maporomoko ya Maji, Bwawa la Kuogelea,
Wanyamapori kama tembo na nyati, mito na manthari nzuri.
Shamba la Miti West Kilimanjaro lilianzishwa mwaka ni 1940 kwa tangazo 227 chini ya sheria ya kikoloni kwa lengo la kuongeza uhifadhi wa vyanzo vya maji na kupunguza tatizo la mmomonyoko wa ardhi katika miinuko inayozunguka Mlima Kilimanjaro.
No comments
Post a Comment