Maliasili na Utalii wapongezwa matumizi mazuri ya fedha za umma
Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo ameipongeza Wizara ya
Maliasili na Utalii kwa matumizi mazuri ya fedha za umma katika utekelezaji wa
miradi ya ujenzi wa lango la kuingilia wageni, barabara ya kilomita 47.2 na
ujenzi wa Picnic Site kwenye Pori la Akiba Mkungunero.
Ameyasema hayo
wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ya kukagua utekelezaji
wa miradi mbalimbali kwenye Pori la Akiba Mkungunero lililopo Wilaya ya Kondoa
Mkoani Dodoma.
“Tuipongeze
Wizara ya Maliasili na Utalii kwa usimamizi mzuri wa fedha hizi za umma ambazo
zinaleta tija katika suala zima la maliasili na utalii hapa nchini,” Sillo
amesisitiza.
Amesema Wizara
ya Maliasili na Utalii ilipata kiasi cha shilingi bilioni 90.2 ambapo bilioni
12.9 ilikabidhiwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na kisha
kiasi cha shilingi milioni 672 kupelekwa Pori la Akiba la Mkungunero kwa ajili
ya kuboresha eneo hilo ili kuvutia wawekezaji na watalii.
Amefafanua
kuwa uboreshaji wa miundombinu ya Pori ya Akiba la Mkungunero utafungua fursa
za utalii nchini Tanzania na pia itaongeza uchangiaji wa Sekta ya Maliasili na
Utalii kwenye pato la Taifa ambapo kwa sasa sekta hiyo inachangia takribani
asilimia 17 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni.
Naye, Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) Wizara ya Maliasili na Utalii
ilifaidika na mgao wa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na
Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambapo ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 88.57
sawa na asilimia 98 ya mpango huo.
Amefafanua
kuwa Pori la Akiba Mkungunero ilitengewa kiasi cha shilingi milioni 672 na
mpaka sasa fedha hizo zimepokelewa zote na zimepangwa kutekeleza miradi mitatu
ambayo ni ujenzi wa lango la kuingilia wageni, barabara ya kilomita 47.2 na
ujenzi wa Picnic Site.
Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Bajeti iko Wilayani Babati na inaendelea na ziara ya kukagua
miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii.
No comments
Post a Comment