Mwaipaya wa CHADEMA aachiwa
Mratibu wa Uhamasishaji wa Baraza la Vijana Chadema
(Bavicha), Twaha Mwaipaya ameachiwa kwa dhamana baada ya kushikiliwa na Jeshi
la Polisi kwa siku tano.
Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa
Morogoro, Jackson Malisa ilieleza kuwa Mwaipaya alikamatwa Alhamisi Juni 30 saa
10 jioni akiwa eneo la Tarminal Pub Msamvu.
Alisema baada ya kukamatwa, uongozi wa Chadema mkoa wa
Morogoro ulienda Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro ambapo walipewa maelezo kuwa
Mwaipaya amekamatwa kwa maelekezo ya jeshi hilo mkoa wa Dodoma na siku
inayofuata angepelekwa Dodoma.
Hata hivyo taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari
na Mawasiliano-Bavicha, Apolinary Boniface imeeleza kuwa Mwaipaya amedhaminiwa
na watu wawili kwa masharti ya kuripoti kituoni Julai 8.
Baada ya viongozi wa chama hicho kupata taarifa ya
kukamatwa Ijumaa na Jumamosi, Mwaipaya hakuonekana Dodoma wala Morogoro na
kuzua wasiwasi kwa familia, ndugu na chama kutoonekana kwake.
Taarifa ya iliyotolewa na Katibu Mkuu Chadema, John
Mnyika ilieleza kuwa chama kimechukua hatua kwa kuwasilisha Habeas Corpus
Mahakama Kuu Dodoma dhidi ya Polisi kumshikilia Mwaipaya kinyume na sheria na
kutaka apewe dhamana au kufikishwa Mahakamani.
Hata hivyo kesi ya maombi madogo ya jinai inayowakabili
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, (AG), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Kamanda wa
Polisi (RPC) na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) Dodoma iliahirishwa baada ya
washtakiwa hao kutofika mahakamani.
Katika shauri hilo la maombi madogo ya jinai namba
25/2022, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiliiomba Mahakama Kuu
kutoa amri ya kuachiwa kwa Mwaipaya.
Akizungumza nje ya mahakama, Wakili wa upande wa
mashtaka, Fredrick Kalonga alidai kuwa Jaji Dk Adam Mambi amefanya busara
kuahirisha kesi hiyo hadi zitakapokwenda mahakamani pande zote mbili.
No comments
Post a Comment