Ivana Trump, mke wa kwanza wa Donald Trump ambaye ni mama wa watoto watatu, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 73.

                  

‘’Alikuwa mwanamke mzuri, mrembo, na wa ajabu, aliyeishi maisha mazuri na ya kutia moyo,’’ Bw Trump alichapisha kwenye mtandao wake wa kijami wa ‘’Truth Social.’’

Bi Trump, ambaye alizaliwa katika nchi ambayo sasa inaitwa Jamhuri ya Czech, aliolewa na rais huyo wa zamani mwaka wa 1977. Walitalikiana miaka 15 baadaye mwaka wa 1992. Walipata watoto watatu pamoja - Donald Jr, Ivanka na Eric Trump.

Polisi wanaamini kuwa sababu ya kifo inaweza kuwa ajali, kulingana na Associated Press.

Vyanzo vya habari vililiambia shirika la habari kwamba Bi Trump alipatikana amepoteza fahamu karibu na ngazi katika nyumba yake ya New York City, na inaaminika kuwa huenda alianguka.

Donald na Ivana Trump walikuwa watu mashuhuri kwa umma huko New York katika miaka ya 1980 na 1990, na mgawanyiko wao ulikuwa mada ya maslahi makubwa ya umma.

Baada ya kutengana, Bi Trump aliendelea kuzindua bidhaa za urembo, nguo na vito.

Alichukua sifa kwa kulea watoto wao katika maandishi ya kumbukumbu yake ya 2017 ‘Raising Trump’, akisema ‘’alifanya maamuzi kuhusu elimu yao, shughuli, usafiri, malezi ya watoto na posho yao’’ hadi chuo kikuu.

Katika kitabu hicho, aliongeza kuwa uhusiano wake na Bw Trump umeimarika tangu talaka yao, na akasema alizungumza naye mara moja kwa wiki.