Siku moja baada ya Ikulu ya White House kutangaza safari ya Rais Joe Biden nchini Saudi Arabia, kundi la wanaharakati lilikusanyika kuubatiza mtaa nje ya ubalozi wake wa Washington "Khashoggi Way".

Walitangaza kuwa itakuwa ukumbusho wa kila siku kwa wanadiplomasia "waliojificha nyuma ya milango hiyo" kwamba serikali ya kifalme ilihusika na mauaji ya 2018 ya mwandishi wa habari wa Saudi na mkosoaji wa serikali Jamal Khashoggi.

Na walishutumu uamuzi wa Rais Biden kukutana na mtu aliyelaumiwa na ujasusi wa Marekani kuwa ndiye aliyeamuru mauaji hayo - Mwanamfalme Mohammed bin Salman, anayejulikana sana kama MBS.

"Ikiwa itabidi kumpaka mtu mafuta zaidi ya kuheshimu kanuni na manufaa ya maadili," alisema mchumba wa Khashoggi Hatice Cengiz katika hotuba yake iliyosomwa kwenye hafla hiyo, "unaweza angalau kuuliza mwili wa Jamal uko wapi? Je, hastahili kuzikwa ipasavyo?"

Mahusiano ya miongo kadhaa ya Marekani na Saudi Arabia yamehusisha biashara kati ya maadili ya Marekani na maslahi ya kimkakati.

 Lakini Rais Biden alisisitiza waziwazi haki za binadamu katika uhusiano huo, na sasa, anapokubali ukweli wa kisiasa, anakabiliwa na hatari ya kupoteza Washington kutokana na hasira ya kitendo hicho. Mwandishi wa habari na mkosoaji mashuhuri wa mwana mfalme  wa Saudia Khashoggi aliuawa na kukatwa vipande vipande katika ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul.

Akiwa mgombea urais, Bw Biden alichora mstari , akiapa kuhakikisha kuwa ufalme huo ‘umetengwa’ kwa sababu ya rekodi yake mbaya ya haki za binadamu. Alitumia maneno hayo makali kujitofautisha na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump aliyeikumbatia Saudi Arabia bila kipingamizi. Bw Trump aliwahi kujigamba kuwa "alimuokoa [MBS'] kutoka kwa kilio cha kifo cha Khashoggi.