Serikali yakabidhi mizinga zaidi ya 300 ya nyuki kwa vikundi na taasisi Ludewa

Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii
imetoa mizinga zaidi ya 300 kwa taasisi na vikundi mbalimbali vya ujasiliamali
wilayani Ludewa mkoani Njombe ili kuweza kuinua uchumi wa taasisi hizo na
wananchi kwa ujumla kupitia ufugaji wa nyuki.
Akikabidhi
mizinga hiyo Waziri wa maliasili na utalii Balozi Dk. Pindi Chana mara baada ya
kufanyika mafunzo ya uhifadhi misitu na vipimo na kusema kuwa shughuli za
ufugaji nyuki zinategemea hasa misitu hivyo endapo ufugaji huo utatendeka vyema
itasaidia kutunza uhifadhi wa misitu na vyanzo vya maji sambamba na kuinua
uchumi wa taasisi na wananchi kwa ujumla kupitia ufugaji wa nyuki.
“Kumekuwa
na uharibifu wa misitu kwa kuchoma mkaa, na matumizi mengine. Hii mizinga ina
faida kubwa sana katika utunzaji misitu pamoja na kukuza uchumi kwa kuwa ili
uweze kufuga nyuki unatakiwa uwe na msitu wa kufugia hivyo hii itasaidia
uhifadhi wa misitu yetu na kupata kipato kupitia asali” Amesema Balozi Dkt.
Pindi Chana.
Dk.Chana
amesema moja
ya wajibu wa Wizara anayoiongoza ni kushirikiana na wanachi ambao ndio wadau wa
kwanza katika uhifadhi endelevu, pia Wizara imeona ipo haja ya kuwapatia
wananchi hao Mizinga watakayoitumia kama chanzo cha mapato pia kuimarisha
ulinzi katika hifadhi za Misitu.
Waziri Chana amewataka
wananchi waliopata mizinga hiyo na mafunzo ya ufugaji nyuki kuitunza na
kuwaelimisha wengine juu ya faida ya Misitu hasa ufugaji Nyuki, hasara
inayotokana na uharibifu wa Misitu pamoja na adhabu ambazo zimeainishwa
kisheria ikiwemo hukumu ya kifungo cha miaka 15 kwa yeyote atakaebainika
kuchoma moto misitu.
Aidha
kwa upande wa mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere ameishukuru wizara hiyo na
kuvitaka vikundi hivyo kuitumia mizinga hiyo katika kukuza uchumi wao kwakuwa
kwa sasa zao la nyuki lipo katika hali nzuri kibiashara.
Ameongeza
kuwa ujio wa mizinga hiyo itakuwa msaada kwa taasisi na wajasiliamali kuwa na
kazi mbadala ya misitu ambapo badala ya kukata miti ili waweze kupata kipato
wataitunza ili waweze kufugia nyuki na kupata faida mara dufu.
Akizungumza
kwa niaba ya wanufaika wa mizinga hiyo Mkuu wa gereza la wilaya ya Ludewa
Johanes Baitange ambaye ofisi yake imekabidhiwa mizinga kumi amesema mizinga
hiyo itasaidia kutoa elimu ya ufugaji nyuki kwa wafungwa na pindi watakaporejea
uraiani wataweza kujipatia kipato kutokana na elimu hiyo walitoipata wakiwa
gerezani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kata ya Ludende, Bi Mariam Mdege amesema mafunzo na mizinga waliyopatiwa licha ya kuimarisha mahusiano bora kati ya wananchi na Serikali itachochea ukuaji wa uchumi kwa jamii huku akiishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwawezesha .


No comments
Post a Comment