Sopu azitolea nje Simba SC, Young Africans
Klabu ya Azam FC inatajwa kumsajili Kiungo Mshambuliaji wa Coastal Union Abdul Seleman Sopu, baada ya kufikia makubaliano binafsi na mchezaji huyo.
Sopu aligeuka lulu katika mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara juzi Jumamosi (Julai 02), akiifunga Young Africans mabao matatu, licha ya Coastal union kupoteza kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.
Azam FC inatajwa kumng’oa kiungo huyo kwa dau la Shilingi Milioni 100, huku klabu kongwe nchini Tanzania Simba na Young Africans nazo zilihusishwa kwenye mkakati wa kuiwinda saini yake, lakini zimezidiwa na matajiri hao wa Chamazi.
Inaelezwa kabla ya Fainali ya ASFC
dhidi ya Young Africans, Sopu alisaini mkataba wa miaka miwili na Coastal kwa dau
la milioni 30, hivyo kuondoka kwake klabuni hapo kutailipa klabu hiyo ya jijini
Tanga.
Kiungo huyo ambaye pia huitwa kwenye
timu ya taifa ya Tanzania *Taifa Stars* mara kwa mara, atasaini mkataba wa
miaka miwili na Azam FC, na atapewa Shilingi milioni 50 kama ada ya usajili.
Azam FC tayari imeshafikisha idadi ya
wachezaji watano waliowasajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya
Kimataifa, wachezaji watatu wanatoka nje ya nchi ni (Issa Ndalah, Kipre Junior
na Tape Edinho) na wachezaji wazawa ni (Cleophace Mkandala na Abdul Sopu).
No comments
Post a Comment