Waandamanaji waliokasirishwa na mkwamo wa kisiasa unaoiandama Libya wamefanya maandamano leo katika wakati kuna wasiwasi wa kusambaa kwa machafuko nchini humo. 

Mkanda wa vidoe uliorushwa kwenye mtandao mmoja wa kijamii umeonesha kundi la vijana wakiandamana usiku kucha nje ya majengo ya Baraza Tawala mjini Tripoli. 

Wengi walibeba mabango ya kuwataka viongozi wa baraza hilo kujiuzulu. Kwenye maeneo mengine ya mji huo, waandamanaji walichoma matairi ya magari huku wakipaza sauti za kutaka kumalizwa kwa tatizo la kukatika kwa umeme kila wakati. 

Maandamano sawa na hayo yameripotiwa pia kwenye mji wa mwambao wa Zliten na mji wa Misrata, magharibi mwa Tripoli. 

Maandamano hayo yametokea siku moja baada ya makundi ya watu wenye hasira kuyavamia majengo ya bunge yaliyo kwenye mji wa mashariki wa Tobruk na kuyachoma moto baadhi ya maeneo. Mvutano wa kuwania madaraka nchini huo ndiyo chanzo cha hasira kubwa ya umma