Tanzania kuandaa AFCON 2027
Tanzania inatarajia kutumia fursa ya
Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika utakaofanyika jijini Arusha
mwezi Agosti, kuthibitisha ipo tayari kuwasilisha ombi la kuwa mwenyeji wa
Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON’ 2027.
Tanzania haijawahi kuwa mwenyeji wa
Fainali hizo tangu zilipoanzishwa mwaka 1957, licha ya kuwahi kupata nafasi ya
kuwa mwenyeji wa Fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019
zilizofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo
Mohamed Mchengerwa ameweka wazi dhamira ya Serikali kwa kushirikiana na
Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ kuwathibitisha utayari wa kuwa mwenyeji kwa
mwaka 2027.
Waziri Mchengerwa aliyasema hayo jana
Alhamis (Julai 07), alipokua akihutubia kwenye hafla ya Utoaji Tuzo kwa Timu,
Wachezaji, Makocha na Waamuzi waliofanya vizuri msimu wa 2021/22 uliofikia
tamati mwezi Juni.
“Mpango wa Serikali ni kuandaa
mashindano ya AFCON 2027 hapa hapa Tanzania na inawezekana. Sera ya michezo
inavitaka vilabu kujenga viwanja vyao vyenyewe.”
“Viwanja vinavyofanyiwa ukarabati na Serikali ni mkakati kwa ajili ya mashindano makubwa. Naomba vilabu viwekeze kwenye kujenga vilabu vyao vyenyewe. Kuna vilabu vipo tangu kabla ya Uhuru, vinashindwaje kujenga viwanja vyao vyenyewe.” Alisema Mchengerwa
Viongozi wa vilabu wawe wabunifu, kama
wanachama wapo tayari kuchanga changisheni.
Naiagiza BMT na TFF waniandalie kikao wiki ijayo na Watendaji wakuu wa vilabu ili tuzungumze kwa nini vilabu vinashindwa kuwa na viwanja vyao vyenyewe.
Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka
Barani Afrika ‘CAF’ umepangwa kufanyika Agosti 10 jijini Arusha, na tayari Rais
wa Shirikisho hilo Patrice Motsepe ameshathibitisha hilo alipozungumza na
Waandishi wa Habari mjini Casablanca-Morocco Jumapili (Julai 03).
Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON’
2023 zitafanyika nchini Ivory Coast na zile za mwaka 2025 zimepangwa kuunguruma
nchini Guinea.
No comments
Post a Comment