Vikundi 51 vya uzalishaji mafuta ya kula Tabora vyakopeshwa mil 107.
Halmashauri
ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imekabidhi hundi ya sh mil 443.3 kwa vikundi
51 vya wajasiriamali wanaojihusisha na uzalishaji bidhaa mbalimbali ikiwemo
mafuta ya kula ya alizeti na mawese.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga
alisema wametoa mikopo hiyo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ili
kuviongezea nguvu vikundi vyote vyenye mwelekeo wa viwanda.
Alisema kati ya vikundi 51 vinavyokabidhiwa mikopo
hiyo vikundi 18 ni vya wanawake na vitapata sh mil 128.2, vikundi 23 vya vijana
sh mil 278 na vikundi 10 vya watu wenye ulemavu sh mil 37.1.
Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo sh mil 195.1
zimetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani na sh mil 243.2 ni fedha za
marejesho ya vikundi vilivyowezeshwa awali ambavyo vimeendelea kufanya vizuri
katika uzalishaji.
Mwaga alibainisha kuwa katika mkopo huo sh mil 107
zimetolewa kwa vikundi vyenye viwanda vidogo vya uzalishaji mafuta ya kula ya
alizeti na mawese na vinavyotengeneza chaki, viatu na sabuni ili kuongeza
uzalishaji wa bidhaa hizo.
Alisisitiza kuwa dhamira yao ni kuona vikundi vya
vijana, wanawake na walemavu vinaleta tija kwenye maendeleo ya wilaya hiyo kwa
kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazogusa maisha ya
wananchi ambazo zitauzwa ndani na nje ya wilaya hiyo na kuinua maisha yao.
Aidha aliongeza kuwa halmashauri hiyo iko mbioni
kuanzisha kiwanda cha kuchakata asali na mazao mengine ya nyuki hivyo akashauri
kuanzishwa kwa vikundi vingi vya wafuga nyuki ili vikopeshwe na kunufaika na
fursa hiyo.
Mwaga alisema kwa sasa wametoa mkopo wa sh mil 17.3
kwa vikundi 2 vya akinamama kwa ajili ya mradi wa kuchakata asali na mazao
mengine ya nyuki kupitia fedha za marejesho na mapato ya ndani.
Alibainisha kuwa kiwanda hicho kitakuwa chachu kubwa
ya kuwaingizia mapato wananchi ikiwemo soko la uhakika la mazao yatokanayo na
asali.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jafael Lufungija
alisema wanataka kuona vikundi vyote vinavyokopeshwa na halmashauri hiyo
vinafanya kazi iliyokusudiwa na kuleta tija kubwa katika uzalishaji bidhaa za
chakula na biashara.
Alitaja changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili kuwa
ni mwamko mdogo wa fursa za ufugaji nyuki, mitaji midogo na kutorejesha mikopo
kwa wakati ila sasa elimu imeanza kutolewa na mabadiliko makubwa yameanza
kuonekana.
No comments
Post a Comment