Wakulima wa mpunga Mbarali watakiwa kuongeza matumizi ya mbegu bora ya TARI
Wakulima wa zao la mpunga wilayani Mbarali Mkoani Mbeya wametakiwa kuongeza matumizi ya mbegu bora zilizotafitiwa na Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mpunga na kuachana na kilimo cha mazoea ambacho tija yake ni ndogo.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Uyole na Mtafiti wa zao la mpunga Dkt. Denis Tippe (mwenye fulana ya kijani) akitoa elimu kwa wakulima kuhusiana na mbegu mpya za zao la mpunga wakati wa maonyesho ya mpunga.
Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Wilaya ya Mbarali Bwana Geoffrey Mwaijobele wakati akifungua maonesho ya Kilimo Biashara cha Mpunga yaliyoandaliwa na Kituo cha TARI Uyole kwa kushirikiana na Vituo vya TARI Dakawa na TARI Ifakara pamoja na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Mpunga(IRRI).
Maonesho hayo yamefanyika katika Kata ya Ubaruku Wilayani Mbarali iliyoko mkoa wa Mbeya.
Katika hotuba yake, Mwaijobele ameipongeza TARI kwa kuleta matokeo ya utafiti wa zao la Mpunga karibu na wananchi hususan katika Wilaya ya Mbarali na kutoa elimu kwa wakulima.
Elimu iliyotolewa katika maonesho ya kilimo biashara cha mpunga ni pamoja na sifa za mbegu mpya za mpunga, maandalizi ya shamba, matumizi bora ya mbolea,palizi na hatua za uvunaji hatua ambayo itasaidia wakulima wa Wilaya ya Mbarali na maeneo mengine yanayofaa kwa kilimo cha mpunga kulima kisasa, kuwa na uhakika wa chakula na ziada ya kuuza kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla .
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Uyole ambaye Dkt. Denis Tippe alieleza kuwa Kituo cha TARI Uyole kiliweka majaribio ya mbegu mpya sita katika skimu ya umwagiliaji Kata ya Ubaruku Wilayani Mbarali ili kuongeza matumizi ya mbegu bora za mpunga na kuliongezea tija baada ya kubaini changamoto iliyopo ya kushuka kwa tija katika uzalishaji wa zao hilo.
Dkt. Tippe aliongeza kuwa mbegu hizo mpya za mpunga za SARO 5, TARI RIC 1 & 2, Komboka, SATO 1 & 9 ambazo zina sifa za kutoa mavuno mengi kuanzia tani 7.5 hadi 8.5 kwa hekta, kunukia, kuwa na punje nzuri, kukomaa kwa muda mfupi na baadhi zinavumilia maeneo yaliyoathiriwa na magadi na chumvi chumvi zimeonyesha kufanya vizuri katika majaribio yaliyoandaliwa kwa ajili ya maonesho hayo ambayo yanalenga mkusaidia mkulima kuchagua mbegu ambayo
itamfaa kulingana na eneo lake.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TARI aliyehudhuria maonesho hayo Dkt. Richard Kasuga amesema maonesho hayo ni moja moja ya majukumu muhimu ya TARI ya kuhakikisha teknolojia zinazotafitiwa zinawafikia wakulima na wadau wa kilimo kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo maonesho ya kilimo biashara, vituo mahiri, vyombo vya habari na mitandao yakijamii.
Aliongoeza kuwa matumizi ya mbegu bora za mpunga zitasaidia kuongeza uzalishaji na hivyo kufikia malengo ya Serikali ya kujitosheleza kwa chakula na pia Malengo ya yaliyoainishwa katika Azimio la Malabo la kukabilana na njaa.
Akizungumzia kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Kasuga ameongeza kuwa katika mwaka wa 2022/2023 bajeti ya maendeleo ya utafiti imeongezeka kutoka takriban bilioni 11 hadi billion 41.
Ameongeza kuwa, Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe ameweka mkazo na malengo ya AJENDA 10/30 yenye kaulimbiu KILIMO NI BIASHARA yenye lengo la kujitosheleza kwa chakula na ziada kwa ajili ya kuuza na kujiongezea kipato, Hivyo maonesho haya ni fursa katika kuwahamasisha wakulima kutumia fursa za masoko ambalo Wizara imeendelea kuyatafuta ikiwemo la Ubeljiji kwa ajili ya kuuza mchele.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wakulima wa zao la mpunga Wilayani Mbarali wameipongeza na kuishukuru TARI kwa kuwezesha kuweka majaribio ya mbegu mpya za mpunga Wilayani humo na kuuomba Uongozi wa Wilaya ya Mbarali kuwaletea wataalamu wa TARI karibu yao ili waweze kuwasaidia kuwapimia afya ya udongo na kuwapa elimu zadi ya matumizi ya mbegu mpya, matumizi sahihi ya
udongo pamoja na ushauri ili waweze kupata tija zaidi katika kilimo chao ikiwa ni pamoja na kuwa na uhakika wa uwepo wa mbegu hizo Wilayani Mbarali.
Wakulima hao wameeleza kuwa muda wote walikuwa wakilima kilimo cha mazoea ambacho hakikuwa na tija kwani walikuwa wakipata gunia 8 -10 kwa ekari moja, lakini sasa wanataka kubadilika na kutumia mbegu mpya za TARI ambazo humuwezesha mkulima kupata kati ya gunia 30 - 40 kwa ekari moja.
Wakulima waliohudhuria maonesho hayo ya Mpunga Kilimo Biashara wametoka katika vijiji vya Ubaruku, Kapunga, Madibila, Uturo na Buyuni Wilayani Mbarali.
Mtafiti Veronica Twisa kutoka Kituo cha TARI Uyole akitoa maelezo kwa wadau waliotebelea maonesho ya mpunga kilimo biashara Wilayani Mbarali.
No comments
Post a Comment