Header Ads

Header ADS

Afisa Mipango Miji ashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za ubakaji .

Jeshi la Polisi mkoani Katavi linamshikilia Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Mpimbwe Dickson Mwenda (37) kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 15 mkazi wa Kibaoni.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi Ali  Makame amesema mtuhumiwa anadaiwa kumbaka mtoto huyo ndani ya gari yake yenye namba za usajili T 927 DMC.
Kamanda Makame alieleza kuwa tukio hilo la unyanyasaji wa kingono lilifanyika tarehe 13 mwezi huu majira ya saa moja na nusu jioni huko katika Kijiji cha Kibaoni, kata ya Kibaoni.
Aliongeza kuwa mama wa mtoto huyo alikuwa baa akipata vinywaji na mtuhumiwa ambapo baada ya muda alimuomba  awapeleke watoto wake nyumbani ambao walikuwa wawili yaani mtoto aliyebakwa na mdogo wake.
Alieleza kuwa mtuhumiwa alipofika njiani alisimamisha gari na kumbaka mtoto huyo.
Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo taarifa zilipelekwa katika kituo cha Polisi na baadae mtuhumiwa alikamatwa.
Aidha Kamanda Makame ameeleza kuwa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na Polisi na atafikishwa mahakama kujibu shtaka lake.


No comments

Powered by Blogger.