Zaidi ya Vijana 130 wamefanikiwa kupatiwa elimu ya ujasiriamali Mkoani Arusha
Zaidi ya vijana 130 kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya ajira, hatimaye wamefanikiwa kupatiwa elimu ya ujasiriamali pamoja na namna ya kujiajiri katika sekta ya viwanda.
Aidha vijana hao wamefanikiwa kupatiwa elimu kupitia mradi wa uanagezi ambapo mradi huo uliibuliwa na Wizara ya elimu sayansi na teknolojia na kudhamiwa na Benki ya dunia na kuratibiwa na SIDO.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mradi wa uanagezi ambao uliwakutanisha wamiliki,pamoja na vijana wajasiriamali mkoa wa Arusha Meneja wa Sido mkoa wa Arusha, Jafari Donge amesema kuwa mradi huo ulidumu kwa kipindi cha mwezi mmoja .
Donge amesema kuwa Sido kupitia mradi huo wameweza kuibua ajira mpya kwa kuwa vijana hao waliweza kupelekwa kwenye viwanda mbalimbali ambavyo vinatekeleza majukumu yao ya kiujasirimali.
“vijana hawa tuliwapeleka kwenye viwanda mbalimbali kama vile viwanda vya usindikaji,saluni,gereji,masuala ya mtandao,mikate,uhandisi,utalii hawa wamiliki wote wapo chini ya Sido na tunashukuru sana wamewapokea kwa muda mfupi wa mwezi mmoja na tayari wameshapata mafunzo huku wengine wakipata ajira za kudumu”amesema.
Aidha Donge amewaasa vijana kuhakikisha kuwa wanatafuta fursa mbalimbali ambazo zinatangazwa ingawaje bado kuna changamoto ya uhaba wa ajira .
Kwa upande wake Mmoja wa wamiliki wa viwanda ,Salma Mnaro alishukuru waandaji wa mpango huo pamoja na Sido kwa kuweza kuwateua vijana ambao walikuwa na uhitaji mkubwa wa ajira na hawana uwezo wa kupata uzoefu wa kumiliki viwanda .
“Napenda kasema kuwa ni muhimu sana kuishukuru Serikali lakini pia Sido kwa kuwa wamekuja na matokeo chanya ambayo wameweza kufungua milango kupitia hata taasisi za fedha .”amesema.
Aliwataka vijana hao ambao muda si mrefu wanaanzisha viwanda vyao kuhakikisha kuwa wanasimama ipasavyo katika ndoto zao za kumiliki pamoja na kusimama katika ubora wa bidhaa ili waweze kuteka soko la dunia.
No comments
Post a Comment