Header Ads

Header ADS

Tanzania na Polandi zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano

 

Serikali za Tanzania na Poland zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali zenye manufaa kwa nchi hizi mbili ikiwemo kilimo, elimu, nishati, utalii, biashara na uwekezaji kufuatia mazungumzo rasmi yaliyofanyika kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Zbigniew Rau.

Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo hayo jijini Warsaw, Poland, Mawaziri hao wamesema Tanzania na Poland ambazo zinaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano, zina fursa nyingi zenye manufaa kwa pande zote mbili na kwamba wamekubaliana kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na kuanzisha ushirikiano kwenye maeneo mapya ya ulinzi na usalama pamoja na nishati.

Amesema, “Katika majadiliano yetu leo, tumetathmini ushirikiano wetu katika maeneo ambayo tayari tunashirikina na Poland kama kilimo, elimu, biashara na uwekezaji na utalii. Pia tumekubaliana kuongeza maeneo ya ushirikiano katika masuala ya nishati na ulinzi na usalama ambayo ni muhimu katika kukuza ushirikiano wetu.”

Katika ziara hiyo, Waziri Tax amefuatana na Wajumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Ukuzaji Biashara na Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Wakala wa Taifa wa Hifadi ya Chakula (NFRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

No comments

Powered by Blogger.