Header Ads

Header ADS

Dkt. Philip Mpango aongoza majadiliano ya mradi wa SGR TZ - DRC

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip

Mpango amesema kutekelezwa kwa mradi wa Reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza
mkoani Kigoma nchini Tanzania hadi Kindu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kupitia Gitega nchini Burundi kutaongeza ufanisi katika matumizi ya Ukanda huru wa
biashara Barani Afrika kwa kuimarisha usafirishaji wa watu na bidhaa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiongoza majadiliano na wawekezaji
kuhusu mradi wa reli hiyo ya kisasa, majadiliano yaliofanyika katika Jukwaa la
Uwekezaji Barani Afrika linalofanyika Jijini Abidjan nchini Ivory Coast. Amesema
serikali zote tatu zimeweka nia ya dhati ya kutekeleza mradi huo ambapo kwa
upande wa Tanzania tayari imekwisha tekeleza miradi unganishi ya reli ya kisasa
inayochagiza uwepo wa mradi huo muhimu.

Aidha Makamu wa Rais amesema asilimia 50 ya mizigo inayotoka katika bandari za
Tanzania hupelekwa nchi za Burundi na Kongo hivyo uhitaji wa reli hiyo ya kisasa ni
muhimu kwa sasa. Amesema uwepo wa idadi watu inayokadiriwa kufikia milioni 170
katika mataifa ya Tanzania, Kongo na Burundi ni uhakika wa soko kwa bidhaa
mbalimbali zitakazosafirishwa kupitia reli hiyo.
 
Pia Makamu wa Rais ameongeza
kwamba mradi huo utaokoa gharama kubwa zinazotumika katika kukarabati
miundombinu ya barabara inayotumika katika usafirishaji wa bidhaa kutoka bandari
zilizopo nchini Tanzania kuelekea mataifa ya Burundi na Kongo.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametaja mradi huo kama njia mojawapo ya kuhifadhi
mazingira kutokana na kutumia nishati ya umeme pamoja na kuimarisha sekta ya
kilimo na bidhaa zake katika ukanda uliojaaliwa ardhi yenye rutuba na rasilimali watu
ya kutosha.
Kwa Upande wake Waziri wa Miundombinu wa Burundi Mheshimiwa Dukundane
Dieudonneè amesema taifa hilo limekuwa likipoteza zaidi ya dola za marekani milioni
17 kila mwaka katika usafirishaji wa mizigo hivyo mradi huo utasaidia katika
kubaliana na hali hiyo. Dukundane ameongeza kwamba mradi huo utasaidia katika
kutumia vema rasilimali za madini zilizopo katika mataifa hayo kama vile dhahabu,
lithium, colbat na nickel kwa kufikisha vema katika masoko ya dunia.

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Adesina Akinwumi amesema
Benki hiyo inaunga mkono kwa dhati utekelezaji wa mradi huo ambao utasaidia
Maisha ya watu barani Afrika. Dkt. Adesina amesema mradi huo ni muhimu kwa
Tanzania , Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla katika ufanyaji biashara na kuinua
uchumi baina ya mataifa katika ukanda huru wa biashara barani Afrika.

Awali katibu mtendaji wa sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika
Wamkele Mene amesema ufanyaji biashara baina ya nchi za Afrika umekua na
changamoto na gharama kubwa kutokana na kutokuwepo na miundombinu rafiki.
Aidha amezipongeza serikali za Tanzania, Burundi na Kongo kwa maono walionayo
katika kutekeleza mradi huo ambao utakua chachu ya biashara katika Ukanda huo
huru wa biashara pamoja na kufikia Ajenda ya Afrika tuitakayo 2063.

Katika Majadiliano hayo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja
Kadogosa amewasilisha mipango ya utekelezaji wa mradi huo kwa wawekezaji
mbalimbali na kueleza mafanikio yaliopatikana katika utekelezaji wa miradi ya awali

ya Reli ya Kisasa nchini Tanzania.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip
Mpango akiongoza majadiliano na wawekezaji kuhusu mradi wa reli ya kisasa (SGR)
kutoka Uvinza Kigoma nchini Tanzania hadi Kindu Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo
kupitia Gitega nchini Burundi, majadiliano yaliofanyika katika Jukwaa la Uwekezaji
Barani Afrika linalofanyika Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.

No comments

Powered by Blogger.