Rais Samia atarajia kufungua kongamano la Dini
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kufungua kongamano kubwa la dini litakalohusisha viongozi mbalimbali wa dini na taasisi zaidi ya 3000 nchini.
Akizungumza wakati akizindua Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Jumuiya (RSMIS), jijini Dodoma, leo, Waziri Masauni amesema kuna malengo mbalimbali ya kufanyika kwa kongamano hilo ikiwemo Serikali kuzitaka taasisi hizo za dini kutoa msaada katika masuala mbalimbali ya kijamii hususani kutengeneza maadili kwa vijana.
“Tumemuomba Mheshimiwa Rais Samia awe mgeni rasmi katika shughuli hii nzito, kimsingi ameridhia na kwa bahati mbaya tumemwambia kwa siku atakayoona yeye inafaa, na yeye akajibu ameridhia na atatujulisha, na pia amenieleza kwa mdomo wake kufarijika na hiyo shughuli na atakuja,” alisema Masauni.
Ameongeza kuwa, “Malengo ya shughuli hii kubwa ni vitu vingi, moja tunataka taasisi hizi za dini zitusaidie katika mambo mengi ambayo tunadhani wao wakifanya kwa nafasi yao vizuri na tukishirikiana vizuri yataweza kutengeneza maadili hususani kwa vijana wetu.”
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa mfumo huo mpya wa kielektroniki wa Usajili na Usimamizi wa Jumuiya nchini, amesema mfumo huo utaondoa dhana potofu uliokuwa umejengeka kwa baadhi ya taasisi dhidi ya msajili wa jumuiya wakidhani kuwa msajili ni mrasimu.
“Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kwa msajili, mengi si ya haki, watu wakidhani kwamba msajili ni mrasimu, mkiritimba, mtu asiyependa maendeleo ya jumuiya hizi, amekuwa akichelewesha usajili, akikwamisha, lakini malalamiko yote haya kwasababu hakukuwa na utaratibu mzuri wa kufuatilia maendeleo ya mambo yao na kwa kupitia mfumo huu changamoto zao zitatatuliwa.” Alisema Masauni.
Alisema mfumo huo pia utasaidia Serikali ukusanyaji wa maduhuli na kila msajiliwa kujua uwezo wake, kujua watu gani wa taasisi hizo waliopo, taasisi zilizosajiliwa kama zimefunguliwa kwa masuala binafsi au zinatumiwa vibaya, na pia mfumo huu utasidia mambo yalikuwa kero kwa taasisi hizo sasa kuonekana wazi.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu, Dkt. Maduhu Kazi aliwapongeza Wataalam wa Tehama kutoka Jeshi la Polisi kwa kuutengeneza mfumo huo na pia kwa kuokoa fedha nyingi za utengenezaji endapo ungetengenezwa na watu wengine ambao siyo watumishi ungekuwa na gharama kubwa.
Naye Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Kihampa, alisema umuhimu wa Mfumo huo kwa Serikali utasaidia kuwezesha wananchi kuwasilisha maombi ya usajili wa taasisi, vyama na vikundi vyenye sifa ya kusajiliwa kuwa Jumuiya bila kulazimika kufika katika Ofisi ya Msajili wa Jumuiya.
“Umuhimu wa Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Jumuiya ‘Registration of Societies Management Information System’ kwa Serikali pia utarahisisha ulipaji wa ada na tozo za Jumuiya kwa urahisi kupitia Mfumo huu na kuthibitisha usahihi wa taarifa binafsi za viongozi na wanachama wa jumuiya za kiraia kuhusu uraia na vibali vya kazi na ukaazi,” alisema Kihampa.
Aliongeza faida nyingine kuwa mfumo utaongeza tija katika usimamizi wa jumuiya kupitia uchambuzi wa utekelezaji wa mashati ya usajili na matakwa ya sheria na kutoa takwimu sahihi na kwa wakati kuhusu Jumuiya za Kiraia zilizosajiliwa na kuonesha idadi ya Jumuiya, aina ya Jumuiya na mtawanyiko wa Jumuiya zote za kiraia zilizosajiliwa nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizindua Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Jumuiya (RSMIS), jijini Dodoma, leo. Mfumo huo utasaidia kuwezesha wananchi kuwasilisha maombi ya usajili wa taasisi, vyama na vikundi vyenye sifa ya kusajiliwa kuwa Jumuiya bila kulazimika kufika katika Ofisi ya Msajili wa Jumuiya. Wapili kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu, Dkt. Maduhu Kazi. Kushoto ni Msajili wa Jumuiya, Emmanuel Kihampa. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wanne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Katibu Mkuu, Dkt. Maduhu Kazi (watatu kushoto), Msajili wa Jumuiya, Emmanuel Kihampa pamoja na viongozi wengine, baada ya kuzindua Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Jumuiya (RSMIS), jijini Dodoma, leo. Mfumo huo utasaidia kuwezesha wananchi kuwasilisha maombi ya usajili wa taasisi, vyama na vikundi vyenye sifa ya kusajiliwa kuwa Jumuiya bila kulazimika kufika katika Ofisi ya Msajili wa Jumuiya. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Kihampa, akizungumza kabla ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kulia) hajazindua Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Jumuiya (RSMIS), jijini Dodoma, leo. Mfumo huo utasaidia kuwezesha wananchi kuwasilisha maombi ya usajili wa taasisi, vyama na vikundi vyenye sifa ya kusajiliwa kuwa Jumuiya bila kulazimika kufika katika Ofisi ya Msajili wa Jumuiya. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi akizungumza kabla ya Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Masauni (wapili kulia) kuzindua Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Jumuiya (RSMIS), jijini Dodoma, leo. Mfumo huo utasaidia kuwezesha wananchi kuwasilisha maombi ya usajili wa taasisi, vyama na vikundi vyenye sifa ya kusajiliwa kuwa Jumuiya bila kulazimika kufika katika Ofisi ya Msajili wa Jumuiya. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza baada ya kuzindua Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Jumuiya (RSMIS), jijini Dodoma, leo. Mfumo huo utasaidia kuwezesha wananchi kuwasilisha maombi ya usajili wa taasisi, vyama na vikundi vyenye sifa ya kusajiliwa kuwa Jumuiya bila kulazimika kufika katika Ofisi ya Msajili wa Jumuiya. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
No comments
Post a Comment