Header Ads

Header ADS

Chongolo atoa wito kwa wazalishaji wa Sukari


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo ametoa mwito kwa wazalishaji wa sukari nchini kuhakikisha sukari inayozalishwa inakwenda kushusha gharama au bei ili kuleta nafuu kwa mlaji.

Chongolo ametoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha sukari Mkulazi kwa ajili ya kusikiliza changamoto, ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza kuzalisha sukari ya kutosheleza ndani ya nchi ni jambo linalokuwa na tija sana.

“Mwito wangu kwenu hakikisheni sukari inayozalishwa inaenda kushusha gharama au bei ya sukari kwa mlaji hilo ndilo jambo la msingi .Sukari sio starehe wala sio hanasa bali ni bidhaa ya matumizi ya mwananchi wa kawaida yoyote yule , mnajua asilimia kubwa ya vyakula tunavyokula vinahitaji sukari viwe vya kiwandani au viwe vya nyumbani kwa hiyo mahitaji ya sukari ni makubwa” amesema Chongolo.

Aidha ameuomba uongozi wa kiwanda hicho kwamba watakapozalisha umeme wao kiwandani hapo maana yake uzalishaji utakuwa wa gharama nafuu na wakianza kuuza umeme wasichukue faida yoyote kuweka mfukoni bali faida hiyo waitumie tena kupunguza gharama ya uzalishaji wa sukari ili baadae ipatikane sukari ambayo itakuwa na bei nafuu kwa ajili ya ununuzi.

Awali Chongolo amezungumzia changamoto ya umeme ambayo amepewa wakati anasomewa taarifa ya kiwanda hicho ambapo pamoja na mambo mengine wamekuwa kwenye mchakato wa kuzalisha umeme megawati 15 ili uweze kutumika kwenye kiwanda hicho.

“Nimefurahi kusikia jitihada ambazo mnazifanya katika kuhakikisha mnakuwa na umeme wenu na kilichonifurahisha mmekwenda mbali zaidi, mnachotaka ni TANESCO kukaa na ninyi mkubaliane, Mmetenga mpaka fedha kwa ajili ya kujenga laini ya kupeleka umeme mpaka Msamvu ili muingize kwenye kituo cha kupokelea pale na kupooza na kuingiza kwenye gridi ya taifa” amebainisha Chongolo

Katibu mkuu wa CCM Daniel Chongolo kwenye Ziara hiyo ameambatana na Katibu wa halmashauri kuu ya CCM Taifa itikadi na Uenezi Sophia Mjema pamoja na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni Issa Haji Gavu kwa ajili ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho pamoja na kuzungumza na Makundi mbalimbali.

No comments

Powered by Blogger.