Header Ads

Header ADS

Wanamichezo wa Urusi wasiruhusiwe kwenye Olimpiki, Zelensky asema

 

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa kuruhusu Urusi kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya 2024 huko Paris itakuwa sawa na kuonesha kwamba "ugaidi unakubalika kwa namna fulani".


Alisema amezungumzia suala hilo na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.


Moscow lazima isiruhusiwe kutumia Olimpiki kwa propaganda, aliongeza.


Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) imesema wanariadha wa Urusi na Belarus wanaweza kushindana bila kuegemea upande wowote katika Olimpiki.


Lakini Ukraine imetishia kususia Paris 2024 ikiwa wanariadha wa Urusi na Belarus wataruhusiwa kushiriki mashindano.


Majaribio ya IOC "kuwarejesha wanariadha wa Urusi katika Michezo ya Olimpiki ni majaribio ya kuuambia ulimwengu kuwa ugaidi unakubalika kwa njia fulani," Bw Zelensky alisema katika hotuba yake ya kila usiku ya video.


Urusi lazima isiruhusiwe kutumia Michezo "au tukio lolote la mchezo kama propaganda kwa uchokozi wake au ubaguzi wa serikali", aliongeza.


IOC ilisema wiki hii kwamba wanariadha wa Urusi na Belarusi wanaweza kushindana kama "wanariadha wasioegemea upande wowote", ikisema kwamba "hakuna mwanariadha anayepaswa kuzuiwa kushiriki kwa sababu tu ya pasipoti zao".


Lakini Bw Zelensky anasema hakuwezi kuwa na kutoegemea upande wowote katika mchezo wakati wanariadha wa nchi yake wanakufa kwenye uwanja wa vita.


Pia alilinganisha na Michezo ya Olimpiki ya 1936 huko Berlin wakati Wanazi walipokuwa madarakani.


Serikali ya Uingereza pia imelaani mpango wa kuruhusu wanariadha kushindana bila upande wowote kama "ulimwengu ulio mbali na ukweli wa vita".

No comments

Powered by Blogger.