Header Ads

Header ADS

Rais Biden kuchunguzwa

  

Mwanasheria Mkuu wa Marekani Merrick Garland amemteua mwanasheria maalum kuchunguza jinsi Rais Joe Biden alivyoshughulikia nyaraka za siri.

Robert Hur, afisa mkuu wa zamani wa idara ya haki wakati wa urais wa Trump, ataongoza uchunguzi huo. Nyaraka zilizopatikana hivi majuzi zilikutwa nyumbani kwa Bw Biden na katika ofisi aliyotumia baada ya muda wake kama makamu wa rais.

Ikulu ya White House ilisema Bw Biden atashirikiana kikamilifu na uchunguzi huo. Kupatikana kwa nyaraka hizo kunaonekana suala la aibu kisiasa kwa Bw Biden, kwani inakuja wakati wa uchunguzi unaoendelea kuhusu madai ya Rais wa zamani Donald Trump na yeye kukutwa na nyaraka zingine za siri.

Kundi la kwanza la nyaraka hizo lilipatikana tarehe 2 Novemba katika ofisi ya Penn Biden, iliyoko huko Washington DC. Kisha zilikabidhiwa kwa Hifadhi ya Kitaifa ya Marekani, Bwana Biden alisema.

Bw Garland alisema kundi la pili la nyaraka hizo zilibainika disemba 20 nyumbani kwa Bw Biden huko Wilmington, Delaware. Aliongeza kuwa Alhamisi asubuhi, mawakili wa Bw Biden waliwaita wachunguzi kuwaarifu kuhusu nyaraka ya ziada, ambayo pia ilipatikana katika nyumba binafsi ya rais.

Baada ya uchunguzi wa awali wa Wakili wa Marekani John Lausch, Bw Garland alisema ofisi yake iliamua kwamba wakili maalum alihitajika kuchunguza jinsi Bw Biden alivyoshughulikia faili hizo kutokana na "hali isiyo ya kawaida" ya suala hilo.

"Uteuzi huu unasisitiza kwa umma kujitolea kwa idara kwa uhuru na uwajibikaji katika masuala nyeti haswa, na kufanya maamuzi bila utata yanayoongozwa na ukweli na sheria pekee," Bw Garland alisema.

Bw Hur alisema atachunguza suala hilo "kwa hukumu ya haki, isiyo na upendeleo".

No comments

Powered by Blogger.