Header Ads

Header ADS

Serikali ya Kidemokrasia ya Congo yalaumu waasi kwa shambulio la Bomu

 



Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewalaumu waasi wenye mfungamano na kundi la Islamic State kwa shambulio la bomu katika kanisa la Pentekoste huko Kasindi, mashariki mwa nchi hiyo.


Watu kumi waliuawa wakati waumini walipokuwa wakienda kwa ibada ya Jumapili, maafisa wanasema.


Takriban watu 39 walijeruhiwa na jeshi la Congo lilieleza kuwa ni "kitendo cha kigaidi" cha Allied Democratic Forces (ADF).


Kundi la ADF ni mojawapo ya vikundi vya waasi vinavyojulikana sana mashariki mwa Congo.


Katika taarifa yake , serikali ya Congo "ilishutumu vikali" shambulio la bomu, ambalo inasema "lilitekelezwa na magaidi wa ADF".


Ilitoa "rambirambi zake za kina" kwa familia zilizofiwa ambao walikuwa wahasiriwa wa "kitendo hiki cha kigaidi cha kudharauliwa".


Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DR Congo umelaani "shambulio la woga na la kuchukiza" huko Kasindi.


Kauli hiyo iliungwa mkono na msemaji wa jeshi la Congo Antony Mualushayi, ambaye alisema: "Ni wazi kwamba hiki ni kitendo cha kigaidi kinachofanywa na magaidi wa ADF ambao wamepata hasara vita na vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo".


Bw Mualushayi aliongeza kuwa "kifaa cha kulipuka" kilitumiwa katika shambulio hilo.


Kasindi iko takriban kilomita 8 (maili 5) kutoka Beni ambapo ADF inahudumu


Mwezi Desemba, mwakilishi mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo aliliambia Baraza la Usalama kwamba Usalama ni "moja ya changamoto kubwa" inayokabili DR Congo.


ADF, kundi la wanamgambo wa Kiislamu, lilianzishwa katika miaka ya 1990 na kimsingi linahusika na malalamiko ya ndani ya Uganda.


Lakini tangu ilipoibuka tena katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - kwa mfululizo wa mashambulizi dhidi ya raia wa Congo na mwelekeo wa kimataifa wa kijihadi - ADF imezidi kudai mashambulizi kwa jina la kundi linalojiita Islamic State.

No comments

Powered by Blogger.