Wanaume wasio na elimu waongoza kwa kumiliki nyumba
Imeelezwa kuwa wanaume wengi wasio na elimu nchini Kenya wanamiliki nyumba kuliko wale wanaume ambao wana elimu za kuanzia vyuo vya ngazi ya kati hadi vyuo vikuu.
Utafiti huo wa masuala ya makazi na afya wa mwaka 2022, uliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Kenya (KNBS), umeonyesha kuwa asilimia 46.7 ya wanaume ambao wanamiliki nyumba hawana elimu rasmi, ikilinganishwa na asilimia 32.2 ambao wana elimu ya kuanzia ngazi ya sekondari hadi vyuo vikuu.
Aidha imeelezwa kuwa asilimia 10 ya wamiliki wa nyumba ni wanawake wasio na elimu rasmi ikilinganishwa na asilimia 3 wenye elimu za ngazi za juu.
Hii imeelezwa kuwa huenda inatokana na mtindo wa maisha ya uhamaji wa vijijini kwenda mijini ambapo Wakenya waliosoma huishia mijini kutafuta kazi, huku wakiishi nyumba za kupanga na wengine kushindwa kumudu kabisa gharama za upangaji, huku wanaume wenzao wanaobaki mashambani hujenga nyumba zao.
Takwimu hizo pia zimeeleza kuwa asilimia 20 ya wanaume wasio na elimu kwa pamoja wanamiliki nyumba na mke ikilinganishwa na asilimia 36.3 ya wenzao wa kike.
Kwa ujumla, asilimia 45 ya wanaume wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49 wanamiliki nyumba ikilinganishwa na asilimia 33 au chini ya theluthi moja ya wanawake walio kwenye umri sawa na wa kwao.
"Wanawake wa vijijini ambao ni asilimia 44 wana uwezekano mkubwa wa kumiliki nyumba kuliko wanawake wa mijini ambao ni asilimia 17, ingawa wanawake wa mijini wana uwezekano mkubwa wa kuwa na hati miliki ya nyumba wanayomiliki kuliko wanawake wa vijijini," zimeeleza takwimu za KDHS.
No comments
Post a Comment