Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linawatuhumu waasi wa M23 kwa kukiuka makubaliano tofauti ya mamlaka ya kikanda ambayo yaliamuru pande zote kusitisha mapigano.

Mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki mbili katika eneo la Masisi karibu na kitovu cha Sake na vitongoji vyake yamesababisha maelfu ya watu kukimbilia miji ya Goma na Minova.

Kanali Ndjike Kaiko Guillaume, mkuu wa jeshi katika jimbo la Kivu Kaskazini, alitangaza kuwa M23 - pia inajulikana kama RDF (Jeshi la Rwanda) - mara nyingi ilikiuka maagizo ya kusitisha mapigano yaliyotolewa na Nairobi, Luanda, na ya mwisho ya Bujumbura.

Mamlaka za Rwanda zinasema kuwa hazina uhusiano wowote na vuguvugu la M23, kwamba hili ni tatizo la DR Congo yenyewe.

Kanali Ndjike alisema: "Ukiukaji wa hivi punde ulitokea siku ya mkutano maalum wa wakuu wa nchi huko Bujumbura", ambapo anasema kuwa M23 ilishambulia kambi za FARDC huko Tuonane karibu na Karenga na Rumeti karibu na mlima wa Mushaki, katika Misa.

Willy Ngoma, mwanaharakati wa M23, aliambia BBC kwamba anachosema Kanali Ndjike ni "unafiki unaofanywa na serikali" kwa sababu "ni vikosi vya serikali na wale waliojiunga na kutushambulia."

Meja Ngoma alisema: “Kwanza tunawaonya dhidi ya kushambulia vituo vyetu, na kuwaua wanaozungumza Kinyarwanda. [Wanaposhambulia] Tunajibu , na tunawafuata ili kunyamazisha silaha."