Waziri, Sulemani Jafo amewataka wagombea wa serikali za mitaa kutoanza kupiga kampeni kabla ya mda uliopangwa
Waziri Jafo hayo amezungumza wakati akitangaza tarehe ya kuanza kuchukua na kurudisha fomu kwa wagombea watakaoshiriki uchaguzi huo ambapo fomu hizo zitaanza kutolewa kesho Oktoba 29 hadi Novemba 4, mwaka huu.
Aidha ameeleza ni jambo la kwaida kwa wagombea kusindikizwa na wafuasi wao na wapambe wao kwa mbwembwe lakini akasisitiza zisiwe kwa staili ya kufanya kampeni.
" Kanuni zetu hazisemi mtu aende kuchukua fomu peke yake, huwezi kumzuia mtu kwenda kuchukua fomu kwa staili anayoitaka lakini staili hiyo isiwe ya kampeni, wagombea wanaweza kwenda na ndugu na jamaa zao lakini niwakumbushe wasifanye kampeni kwa kuwa muda bado haujatangazwa rasmi," Amesema Waziri Jafo.
Lakini pia ameeleza kuhusu Kuhusu hofu ya baadhi ya maeneo kutokua na watendaji watakaosimamia uchaguzi, Mhe Jafo amesema changamoto hiyo ishafanyiwa kazi kwa baadhi ya Maafisa Tarafa kuteuliwa lakini pia kama ulivyo utaratibu sehemu ambayo haina mtendaji yupo ambaye atakaimu.
" Kwa mujibu wa kanuni zetu suala la uchukuaji fomu litaanza kesho Oktoba 29 na litakoma Novemba 4, hiki ni kipindi muhimu sana kwa wagombea kwani zoezi hilo litadumu kwa siku Saba,Lakini pia nimetoa ufafanuzi na muongozo kuwa siku ya kuchukua fomu siyo hiyo Oktoba 29 tu Bali mgombea anaweza kuchukua fomu hata tarehe 30 kikubwa ni asipitishe Novemba 4 awe ameirudisha," Amesisitiza Waziri Jafo.
Hata hivyo Waziri Jafo Amesema anaamini kuwa watanzania wote wenye sifa za kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi huu watajitokeza kuchukua fomu kwani huu ndio muda wa kuweza kufanya hivyo kupitia vyama vya vya Siasa vyenye usajili wa kudumu.
Amewataka wagombea na viongozi wao wa vyama kuzingatia kanuni na taratibu za uchaguzi hasa katika suala la kuchukua na kurudisha fomu ili kusije kuleta mkanganyiko hapo baadae.
" Nichukue fursa hii kuwashukuru sana Watanzania toka tumeanza zoezi la kujiandikisha hadi sasa tunavyoenda kwenye hatua ya kuchukua fomu wameendelea kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwenye kila hatua. Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania mwenye haki ya msingi ya kushiriki uchaguzi huu anashiriki bila kuwepo kwa malalamiko yoyote," Amesema Jafo.
Hali Kadharika,Waziri Jafo amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ndio Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye maeneo yao kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi huo ambao itafanyika Novemba 24 mwaka huu.
Imeripotiwa na Mwandishi wetu;Elyudi Kihwele
No comments
Post a Comment