Header Ads

Header ADS

Waziri Mhandisi Isack Kamwelwe,afungua mafunzo ya udereva kwa wanawake.

        Mhandisi Isack Kamwelwe,ambae ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amefungua mafunzo ya udereva kwa wanawake 102 yatakayofanyika katika Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) jijini Dar es Salaam.
     Ambapo amesema lengo la kufungua mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanawake kuwa madereva mahiri wa mabasi na hivyo kuwa chachu katika kuboresha usafiri nchini.
   Akifungua mafunzo hayo ya siku arobaini na tisa yanayofadhiliwa na Benki ya Dunia, na kuratibiwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Waziri Kamwelwe, amesema kuwa mpango huo wa mafunzo umekuja wakati muafaka kwani Serikali inahitaji wataalamu wenye weledi katika miradi ambayo inaendelea kutekelezwa hapa nchini. 















     “Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuijenga Nchi ya Uchumi wa Viwanda ambapo imewekeza nguvu kubwa katika kuboresha na kuimarisha miundombinu ikiwemo upanuzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha, ujenzi flyover ambayo imekamilika, ujenzi wa interchange Ubungo, pamoja na Mradi wa Mabasi yaendayo kwa Kasi (BRT) na hivyo miundombinu hii inahitaji madereva wenye ueledi katika kuilinda na kuiendeleza”, amefafanua Waziri Kamwelwe.
      Lakini hata hivo ameongeza kuwa  fursa hiyo imetolewa kwa wanawake kwa kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa madereva wanawake ni makini zaidi wawapo barabarani. “Nimefanya kazi kwa miaka mingi lakini sijawahi kuona au kusikia mwanamke amefika ofisini akiwa amelewa hivyo naamini tunaandaa wataalam wenye maadili na kazi yao”, amesema Waziri Kamwelwe. 
      Aidha,amesema kuwa  kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana katika kuimarisha usalama wa usafiri kwa njia ya barabara kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi yetu.
   Awali akitoa taarifa Mkuu wa Chuo cha NIT, Mhandisi Prof. Zacharia M.D. Mganilwa, amemueleza Waziri huyo kuwa Chuo kimepanga kuendelea na mafunzo hayo pamoja na kuanzisha mafunzo ya waendesha mizani ili kusaidia kupunguza changamoto za kukosa watalaamu mahiri wa masuala hayo.
     Kwa upande wake Gilliard Ngewe ambae ni  Mkurugenzi Mkuu wa LATRA amesema ana imani kuwa madereva hao watakapomaliza mafunzo hayo watakuwa waaminifu, wadilifu na wazalendo katika kulinda rasilimali ambazo watanzania kupitia kodi zao wamewekeza ili kuchangia maendeleo ya Taifa letu. 
   hata hivo Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Taifa Fortunatus Muslim, amesema kuwa mpango huu umekuja wakati muafaka ambapo nchi inaelekea kukua kuelekea uchumi wa kati na kupanua miundombinu yake. 
    Ambapo ameongeza kwa kusema kuwa ni wakati sasa wa kutoa uelewa kuwa udereva ni taaluma na sio kimbilio la wale waliokosa ajira kwani taaluma hiyo inabeba maisha ya watu. Ameongeza kuwa ana imani wanawake waliochaguliwa wataleta mabadiliko makubwa kwani tafiti zinaonyesha kuwa katika ajali 110 madereva waliopoteza maisha walikuwa madereva 109 ni wanaume na dereva mmoja ni mwanamke.

No comments

Powered by Blogger.