Makamba aanzisha majadiliano Mradi wa Liquefied Natural Gas-LNG
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ameanzisha majadiliano ya utekelezaji wa mradi wa gesi ya kimiminika (Liquefied Natural Gas-LNG) baina ya Serikali na Kampuni za Shell Tanzania ambao ni wawekezaji katika vitalu namba 1 na 4 na Equinor ambao ni wawekezaji katika kitalu namba 2
Makamba akizungumza mara baada ya kufungua kikao cha majadiliano Jijini Arusha, Makamba alisema “Serikali imedhamiria kwa dhati kuendeleza shehena kubwa ya gesi asilia iliyogundulika katika kina kirefu cha bahari kwa kuwa na mradi wa LNG ambao utawezesha kuivuna na kuiuza gesi hiyo kwa soko la kimataifa na pia kuhudumia mahitaji yetu ya ndani na yale ya kanda”.
Katika mazungumzo yake Makamba aliongeza kuwa mradi wa LNG ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati ambapo mradi huu unakadiriwa kugharimu shilingi Trilioni 70 za Kitanzania na kuzalisha ajira zaidi 7000.
Kwa upande wao Wawakilishi wa Makampuni ya Shell na Equinor, Bi. Uni Fjær ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa Equinor Tanzania na Ndg. Jared Kuehl ambaye ni Mkurugenzi Mkazi kutoka kampuni ya Shell walieleza utayari wa makampuni yao kutekeleza mradi huu mkubwa kwa maslahi ya pande zote. Bi. Uni alisema “Equinor ina dhamira ya dhati kuona mradi huu unatekelezeka kwa wakati kwa faida ya pande zote”. Nae Ndg. Jared kutoka Shell alisema “ Shell pamoja wabia wake inafuraha kuona majadiliano ya kutekeleza mradi wa LNG yameanza tena na tunaamini kwa pamoja tutafikia malengo tuliyojiwekea”
Mradi wa LNG unahusisha uvunaji wa gesi iliyogunduliwa baharini na kuibadili kuwa kimiminika ili kuweza kuisafirisha kwa urahisi kwa ajili ya kuuza katika masoko ya kimataifa na sehemu ya gesi hiyo pia itatumika kuhudumia mahitaji ya ndani na yale ya Kanda ya Afrika Mashariki na Kati. Mradi huu utajengwa Mkoani Lindi ambapo Serikali kupitia TPDC tayari ilishatwaa eneo na kulipa fidia wananchi katika eneo hili tayari kwa kuanza kutekeleza mradi pale majadiliano yatakapokamilika.
No comments
Post a Comment