Serikali imefungulia Magazeti yaliyokuwa yamefungiwa
Serikali imeyafungulia rasmi magazeti manne ambayo ni Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima yaliyokuwa yamefungiwa kwa muda mrefu.
Uamuzi huo umetangazwa leo Alhamisi, Februari 10, 2022 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari na kutoa leseni ya magazeti hayo.Amesema nia ya Serikali ya awamu ya sita ni njema ya kutengeneza na kujenga mahusiano mazuri na waandishi wa habari.
Waziri Nape amesema “
"Leo nitatoa leseni kwa magazeti manne yaliyokuwa yamefungiwa ambayo ni Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima" amesema Waziri Nape wakati akitangaza kuyafungulia magazeti hayo huku wahariri wakishangilia.
Pia, Nape ameagiza Idara ya Habari Maelezo kwa kushirikiana na wahariri na taasisi zingine za habari ndani ya muda mfupi kuandaa kikao cha wadau wa habari kuzungumza marekebisho yaliyopelekwa Serikalini ya sheria ya habari.
“Kwenye hicho kikao mwisho wake tutatengeneza kamati ndogo ambayo itatokana na waandishi wa habari tushauriane tupitie kifungu hadi kifungu tuone ni namna gani wapi tunakubaliana halafu tupeleke marekebisho bungeni ya kupitia upya sheria ya habari.
“Mimi nikiwa Waziri nakumbuka nilisimamia sheria ile, mazingira ya wakati ule tofauti na sasa, kwahiyo tutaipitia tutakubaliana yatakayowezekana kubadilika tutabadilisha kwasababu ni maaagizo ya Rais. Haya mazungumzo hayafanyi sheria isimame baadhi ya mambo lazima yaendelee, yale yenye utata lazima tuyape muda mfano lile la elimu lilikuwa na utata basi tuongeze mwaka mmoja wakati tunaendelea na mazungumzo,” amesema.
No comments
Post a Comment