Header Ads

Header ADS

Ukosefu wa miundo mbinu kwa wakulima na wafugaji chanzo cha migogoro.


Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro itaendelea kukabiliwa na migogoro ya wakulima na wafugaji iwapo hatua stahiki za uwekwaji wa mazingira rafiki kwa wafugaji na wakulima katika kutekeleza shughuli zao hazitachukuliwa. 

Afisa Programu wa Mradi wa Uhakika wa Maji (Fair Water Future ) unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Shahidi wa Maji Bwana Tondelo Gungulundi akizungumza na wafugaji wa Kijiji cha Bwade wilayani kilosa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya kazi za Mashahidi wa Maji.

Hayo yametokana na mfano hai wa kijiji cha Bwade Wilayani humo ambacho kinakabiliwa na migogoro hiyo kutokana na ukosefu wa majosho na malambo hali inayowalazimu kutembea umbali mrefu na Mifugo kufuata maji Kupitia kwenye mashamba ya wakulima hali inayosababisha migogoro kati yao na wakulima.

Wakizungumza kwenye ziara ya kikazi iliyofanywa na Afisa Programu wa Mradi wa Uhakika wa Maji (Fair Water Future ) unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Shahidi wa Maji Bwana Tondelo Gungulundi wenye lengo la kukagua maendeleo ya kazi za Mashahidi wa Maji katika kijiji hicho.

Wafugaji hao walisema licha ya kuwa na visima viwili vinavyohudumia mifugo na binaadamu bado Wana uhitaji wa malambo kwani wamekuwa wakitumia muda mrefu katika kupeana  zamu ya kunywesha mifugo hali inayowalazimu kuswaga ng’ombe na kwenda kunywesha mto Ilonga ambao na wenyewe umeathirika na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuwepo kwa mashamba ya wakulima.

Aidha wafugaji hao akiwemo Bi Neema Leboi ambaye  alisema  wamekuwa wakipoteza mifugo mengi kipindi cha kiangazi hasa  ng’ombe kwa sababu ya kukosa maji na malisho hali inayopelekea  ugumu wa maisha.

“Ng’ombe wanateseka sana wakati wa kiangazi kwa kukosa maji wanakaa kuanzia asubuhi mpaka jioni na wakati mwingine wanashindwa hata kwenda kula kwa kusubili foleni ya maji.” Alisema bi Neema.

Kwa  upande wake kiongozi wa kimila jamii ya wamasai (Leigwanani) katika Kijiji cha Bwande Bwana Ibrahim Kindeti alisema pamoja na changamoto ya maji na malisho inayowakabili wafugaji hao pia kuna mgogoro wa ardhi kati yao na wakulima unaosababishwa na wakulima kuingia kwenye maeneo ya malisho ya wafugaji.

Aidha ameiomba serikali ya Wilaya ya Kilosa kuwafukulia malambo yaliofukiwa na mafuriko ili kuwaondolea adha ya kuhama kutoka kijiji kimoja kwenda kingine na kusababisha migogoro ya wakulima na wafugaji.

Pia amewataka wafugaji kuacha tabia ya kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima kwani kufanya hivyo ni kosa na atakayebainika anafanya kitendo hicho atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Nae Afisa Programu wa Mradi wa Uhakika wa Maji (Fair Water Future ) Bwana Tondelo Gungulundi alisema mradi huo unalenga kutoa elimu kwa wananchi ya namna wanavyoweza kujisimamia na kuwasilisha changamoto zao kwa viongozi wa serikali kwa njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari na kuandika barua kwa viongozi hao.

Pia  amewaomba viongozi wa  serikali kusikiliza na kutatua changamoto zinazoibuliwa na wananchi hasa wa vijijini kwani wamekuwa changamoto nyingi zinazoshindwa kufika kwa viongozi hao kutokana na uwoga wa wananchi. 

Afisa Programu wa Mradi wa Uhakika wa Maji (Fair Water Future ) Bwana Tondelo Gungulundi akikagua maziwa aliyopewa kama zaidi na wanawake wa jamii ya kimaasai katika Kijiji cha Bwade wilayani kilosa alipofanya ziara katika kijiji hicho ya kukagua maendeleo ya kazi za Mashahidi wa Maji.


No comments

Powered by Blogger.