Bunge la Urusi limeidhinisha mswaada wa sheria unaoiruhusu serikali kuteuwa uongozi mpya kwenye kampuni za kigeni ambazo zimejiondowa nchini humo baada ya uvamizi wake dhidi ya Ukraine. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali, TASS, sheria hiyo mpya itahamishia udhibiti wa kampuni ambazo zimeondoka Urusi sio kwa sababu za kiuchumi, bali kwa "sababu ya chuki dhidi ya Urusi barani Ulaya na Marekani." TASS imesema wamiliki wa kigeni bado wataweza kurejesha shughuli zao ama kuuza hisa zao. Kampuni nyingi za kigeni zimesitisha shughuli zake nchini humo, huku nyengine zikiondoka moja kwa moja licha ya mitaji mikubwa waliyowekeza. 

Mwezi huu, kampuni ya chakula ya McDonald's ilitangaza kwamba inauza mikahawa yake 850 nchini Urusi. Mswaada huo uliopitishwa na baraza la Duma katika bunge la Urusi, utapaswa kwenda kwenye baraza la juu na kisha kusainiwa na rais kuwa sheria kamili.