Wakuu wa mikoa wapewa agizo anuani za makazi
Waziri wa habari,
mawasiliano na teknolojia ya habari, Nape Nnauye amewataka wakuu wa mikoa yote
nchini kufanya uhakiki wa takwimu za operesheni ya anuani za makazi katika
mikoa yao hasa kipengele cha usimikaji wa miundombinu ya nguzo zenye majina ya
barabara na mitaa pamoja na namba za nyumba.
Akizungumza kwenye
kikao kazi na wakuu wamikoa kilichofanyika jijini Dodoma, waziri Nape amesema
uhakiki huo ni muhimu kwa takwimu za usimikaji wa miundombinu hiyo zinaonesha
zipo chini ukilinganisha na uhalisia wa kilichotekelezeka mikoa ambayo kwa nyakati
tofauti yeye binafsi pamoja na viongozi wengine walipita kukagua na kuridhika
na utekelezaji.
Amesema ifikapo mei 27
wizara hiyo itakuwa imepeleka fedha kwenye mikoa yote kwa ajili ya kufanya
uhakiki na kuweka takwimu sawa kulingana na uhalisia, ili taarifa
itakayowasilishwa ikiwa imesainiwa na mkuu wa mkoa husika iwe na sahii na ndio
itakayokabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake katibu
mkuu wa wizara ya habari, mawasiliano na teknolojia ya Habari, Dk.Jim Yonazi
amesema kazi ya utambuzi wa makazi ya watu ni moja ya eneo muhimu
litakalosaidia nchi kuingia kwenye uchumi wa kidigitali, ambao hauna mipaka na
unaoruhusu wananchi kujihusisha na shughuli za kiuchumi mahali walipo.
No comments
Post a Comment