Wizara ya maji ameuagiza Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) kupanga bei elekezi ya maji katika maeneo ya vijijini ili kuwapunguzia mzigo wa gharama za ununuzi wa maji.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso katika kikao kazi cha watendaji wa wizara na mamlaka zilizochini yake.

Aweso amesema bei ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ni Sh1600 kwa unit moja ambayo ni sawa na Sh30 kwa ndoo moja yenye ujazo wa lita 20 za maji.

Amesema bei ya unit moja ya maji vijijini ni Sh2,500 kwa unit moja ambayo ni sawa na Sh50 kwa ndoo moja ya maji yenye ujazo wa lita 20.

“Inakuaje wa vijijini anunue maji kwa Sh50 inamaana unit moja ananunua zaidi ya Sh2500. Ruwasa watoa bei elekezi kwa wananchi wa vijijini. Mfano dizeli watakuwa na bei yao, umeme wa jua bei yao na umeme (wa kawaida) bei yao,”amesema.

Hata hivyo amesema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kumpunguzia mzigo mwananchi wa vijijini na kwamba utekelezaji wa maelekezo hayo hautachukua muda mrefu kuanza.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha kuanza utekelezaji wa bajeti ya 2022/2023 ambacho ni Julai, 2022 watakuwa wametoa maelekezo hayo na namna gani mwananchi huko vijijini aweze kupata huduma ya maji kwa bei nafuu.

Aidha, Aweso amewataka watendaji wa mamlaka za maji kutochukua muda mrefu kuanza utekelezaji wa miradi ya maji.

“Usianze tena kutumia muda mrefu michakato inayohusiana na manunuzi juu ya utekelezaji wa miradi ya maji. Michakato hiyo ianze sasa hivi sio wakandarasi wapatikane Desemba,”amesema.

Ameagiza michakato hiyo kuanza sasa hivi ili wanapoingia katika mwaka mpya wa fedha miradi hiyo inaanza utekelezaji wake.

“Tunahitaji mkandarasi mwenye uwezo apatikane kwa wakati kwasababu tunauhakika wa fedha juu ya upatikanaji wake. Kwa hivyo hatuna sababu hata moja ya ucheleweshaji wa miradi ya maji,”amesema.

Aidha amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023, watatekeleza miradi ya kimkakati 175 mijini na miradi 1163 vijijini.

Pamoja na hayo amesema mwananchi anatakiwa kupatiwa maunganisho ya maji ndani ya siku saba na kuwaagiza viongozi wa mamlaka za maji kusimamia hilo.