Ndege ya kwanza kuelekea Rwanda ikiwa na wahamiaji wanaovuka kivuko cha bahari cha English Channel inatarajiwa kuondoka katika muda wa wiki mbili tarehe 14 Juni, Ofisi ya Mambo ya Ndani imesema.

Maafisa wameanza kutoa maelekezo rasmi kwa watu wa kwanza kupelekwa katika nchi hiyo ya Afrika

Inatarajiwa kutakuwa na changamoto za kisheria dhidi ya hatua hiyo.

Mpango huo wenye utata umekosolewa na wanasiasa, mashirika ya misaada na Askofu Mkuu wa Canterbury ambaye aliuita kinyume cha asili ya Mungu.

Chini ya mpango huo, baadhi ya waomba hifadhi ambao wamewasili Uingereza wanatumwa Rwanda ambako maombi yao yatashughulikiwa.

Wakati maombi yao yanazingatiwa watapewa malazi na usaidizi na, ikiwa watafaulu, wataweza kusalia Rwanda na kupata elimu na usaidizi wa hadi miaka mitano.

Katibu wa Mambo ya Ndani Priti Patel alisema ushirikiano na Rwanda ni "sehemu muhimu ya mkakati wetu wa kurekebisha mfumo uliovunjwa wa hifadhi na kuvunja mtindo wa biashara ya watu waovu-waingizaji wa magendo".