Kesi yanguruma Mwaikali akipinga kusimikwa askofu mpya wa Konde
Hatimaye kesi ya Dk Edward Mwaikali askofu
aliyeondolewa katika Dayosisi ya Konde ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) kupinga kusimikwa kwa askofu mpya, Geofrey Mwakihaba imeanza
kuunguruma.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa juzi katika
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, mbele ya Jaji James Karayemaha ambapo wawasilisha
maombi walieleza sababu ya kupinga kusimikwa kwa Mwakihaba.
Wakili anayeuwakilisha upande wa Mwaikali,
Godwin Mussa alieleza sababu za pingamizi hilo kuwa ni kulinda haki ya mtu
mmojammoja ili kuepuka vurugu zinazoweza kujitokeza wakati wa kusimikwa kwa
askofu mteule hapo Juni 5.
“Mheshiniwa jaji endapo hakutakuwapo zuio
lolote, Kanisa la KKKT litakuwa likiongozwa na maaskofu wawili kwa kuwa
kuondolewa kwa Askofu Mwaikali hakukufuata taratibu na kanuni za katiba ya
kanisa,” alisema.
Wakili Mussa aliongeza kuwa migogoro iliyopo
kwenye jamii ni mikubwa hivyo ni vyema mahakama ikarejea maombi
yaliyowasilishwa ikiwa ni pamoja na kupinga kulazimishwa kurejesha vifaa vya
Askofu Dk Mwaikali.
Aidha aliiomba mahakama kuangalia pingamizi
la kisheria kwamba mleta maombi, Askofu Mwaikali alituhumiwa bila kupewa nafasi
ya kusikilizwa na kutolewa katika nafasi yake bila kufuata taratibu, kanuni na
katiba ya Dayosisi ya Konde.
Wakili Mussa aliongeza kuwa mahakama ina haki
ya kusikiliza maombi yaliyowasilishwa kwa kuwa ni chombo chenye kutoa haki na
si kuingilia migogoro ya kidini.
Akijibu maombi hayo, wakili wa wajibu maombi,
Dk Daniel Palangyo aliiomba mahakama kulitupilia mbali ombi hilo kwa kuwa
Askofu Mwaikali hakufuata taratibu za kanisa kufungua kesi mahakamani hapo.
Aidha alimtaka mleta maombi awasilishe
vielelezo mahakamani kwa nini hakulalamika kwenye Mkutano Mkuu wa Kanisa chini
ya kifungu cha Sheria 13 cha mwaka 2015.
Alisema hawapingani na hoja ya Mwaikali bali
wanamshauri afuate utaratibu uliowekwa chini ya katiba ya kanisa kabla ya
kulipeleka shauri hilo mahakamani.
“Mahakama ione hoja ya msingi ya kuyatupilia
mbali maombi hayo na mleta maombi atatakiwa kulipa gharama,” alisema.
Baada ya kusikiliza maelezo ya panda zote,
Jaji Karayemaha aliwataka viongozi hao wa dini kutotengeneza chuki na maneno
yanayowasilishwa mahakamani yazingatie vifungu vya Biblia.
Alisema wanapaswa kukaa meza moja kulinda
amani na kufanya maamuzi mazuri na kuachana na chuki, maneno makali kwa kuwa
wao ni wamoja na ipo siku watadumu pamoja.
Jaji Karayemaha alisema ufike wakati
washirikiane na vyombo vya dola hususani Jeshi la Polisi kuitafuta amani,
kutathimini utu na kufurahia maisha.
Jaji huyo alihairisha kesi hiyo mpaka kesho
itakapotajwa tena na kuanza kupitia maombi ya pingamizi lililotolewa.
No comments
Post a Comment