Polisi yatupiwa lawama tisho la bunduki
Tukio la kutishiwa bastola kwa Kisumo Msangi hadharani kisha kumalizwa kituoni kimyakimya, limeacha lawama kwa Jeshi la Polisi mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa, Martin Otieno aliahidi kufafanua kuhusu
tukio hilo lililotokea Desemba 30 mwaka jana na kuripotiwa kituo cha polisi kwa
DOM/RB/14863/2021, lakini hakufanya hivyo.
Wakati linatokea, aliyekuwa kamanda wa Polisi Dodoma, Onesmo
Lyanga aliagiza mhusika akamatwe, lakini aliachiwa siku iliyofuata.
Chanzo cha ugomvi huo ni Msangi kununua nyumba iliyokuwa
inamilikiwa na Iman Ilomo kwa mnada wa mahakama kutokana na deni la benki
alilokuwa akidaiwa, lakini mhusika hakukubaliana na bei iliyouzwa.
Siku ya tukio, inaelezwa Msangi akiongozana na ndugu zake pamoja
na balozi wa mtaa, Tisa Msoso ghafla alitokea Ilomo na kumnyooshea bunduki huku
akimwamuru asali sala yake ya mwisho.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Abinery Alex alisema hofu
ilitanda kiasi cha akina mama kupiga mayowe kwa hofu ya kutokea mauaji.
“Tulipiga simu polisi ambao walifika dakika chache na kumkamata
mhusika akiwa na bunduki mkononi. Walisema risasi iligoma kutoka, vinginevyo
angemuua mbele yetu, jambo la ajabu eti kesi imeisha kinamnanamna tu, polisi
Mungu anawaona jamani,” alisema.
Kwa upande wake, Msangi alikiri kutokea kwa tukio hilo akisema
nyumba aliinunua kisheria ila anashangaa ukimya wa polisi uliodumu kwa miezi
mitano sasa.
“Tulikuwa na ugomvi mkubwa kwenye nyumba hata nimeamua kuilipia
mara mbili, maana pesa zinatafutwa lakini roho haitafutwi, kwa hiyo huko
tumemalizana mimi nimekula hasara kwa mara ya pili, hili la
bunduki…linanikumbusha maumivu, namuachia Mungu,” alisema Kisumo.
Naye Msoso alisema haelewi kilichofanyika hata polisi wakaamua
kulimaliza tukio hilo kubwa kimyakimya.
“Binafsi ni tukio kubwa la kwanza kulishuhudia, nashangaa hata
siku moja polisi hawajawahi kuniita nitoe ushahidi, kwa hiyo inaonyesha
lilimalizwa kwa mazingira wanayojua wao,” alisema Msoso, balozi wa mtaa
lilikotokea tukio hilo.
No comments
Post a Comment