Mwalimu aliyejifungua mapacha wanne Tunduru sasa kuhamishiwa mjini
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro
amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kumhamishia shule
ya mjini Mwalimu Judith Sichalwe (29,) ambaye amejifungua mapacha wanne.
Mtatiro ametoa maagizo hayo baada ya
kumtembelea Mwalimu huyo katika kijiji cha Mkapunda kilicho umbali wa kilomita
100 kutoka Tunduru Mjini, na kusema Serikali itakuwa jirani na Mwalimu huyo ili
kujua maendeleo ya afya yake na watoto.
Amesema ni wajibu wa Serikali kumpa usaidizi
utakaompa nafuu mwalimu huyo, kwani upo uwezekano wa kushindwa kumudu gharama
za maisha kutokana na kupata idadi ya watoto wachanga wanne kwa wakati mmoja na
kuwataka Watanzania watakaouguswa na tukio hilo kutoa msaada ili aweze
kuwatunza.
“Watanzania watakaoguswa kumsaidia Mwalimu
Judith wasisite kuwasiliana naye kupitia namba 0673 103 536 iliyosajiliwa kwa
majina Judith Sichwale, kwani anahitaji msaada kutokana na idadi ya watoto
aliowapata na maziwa ya mama pekee hayataweza kutosha kuwahudumia wote,”
amesema Mtatiro.
Awali, akiongea baada ya kutembelewa na ugeni
Mwl. Judith amesema, amepata mapacha wanne wawili wakiwa ni jinsia ya kiume na
wawili wakike na kwamba alijifungua kwa njia ya kawaida katika Hospitali ya
Misheni ya Mbesa iliyopo Mkoani Mkoani Ruvuma.
“Namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha
kujifungua salama,vlakini kutokana na mahitaji makubwa ya watoto, nawaomba wasamaria
wema wanisaidie mahitaji mbalimbali kama fedha na maziwa ili niweze kuwalea
hawa watoto,”amefafanua Mwalimu Chawe.
Tayari upande wa watumishi wenzake wameanza
kujitolea kwa kujichangisha kiasi cha fedha, ili Mwalimu huyo aweze kumudu
jinsi ya kuwalea watoto hao ambao wanahitaji uangalizi wa karibu na chakula
katika ukuaji wao.
No comments
Post a Comment