Serikali kuzingatia sheria za kimataifa, kuheshimu haki za binadamu
Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa nchini kuwa inazingatia na
kutekeleza sheria za kimataifa za haki za binadamu huku ikiendelea kulinda
uhifadhi wa eneo la Ngorongoro.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb)
jana Jijini Dar es Salaam alipozungumza na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya
Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kuwaelezea mpango wa Serikali katika
kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.
“Napenda kuchukua nafasi hii
kuuhakikishia umma wa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania
inazingatia na kutekeleza sheria za kimataifa za haki za binadamu na hakuna
nanma itaendesha mipango yake kwa kukiuka sheria za haki za binadamu”, alisema
Balozi Mulamula.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa
Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza mpango wa kulinda na
kuhifadhi eneo la Ngorongoro nchini kwa wananchi kuridhia kuhama kwa hiari yao
na kwamba hakuna aliyeondolewa katika eneo hilo kwa nguvu kama inavyoelezwa.
“Tanzania siku zote italinda watu
wake, maliasili zake na mipaka yake kwa kuzingatia sheria za kimataifa,”
alisema Balozi Mulamula.
Akizungumza katika kikao hicho maalum
kwa ajili ya kuielezea Jumuiya ya Kimataifa iliyopo nchini, Waziri wa Katiba na
Sheria Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amesema kinachoendelea katika eneo la
Ngorongoro kwa wakati huu ni uhamaji wa hiari wa wananchi waliokuwa ndani ya
eneo la Ngorongoro na sio kwamba kuna uhamishaji wa nguvu unaofanywa na
Serikali.
“Serikali imekuja na mpango wa
kulinda eneo la Ngorongoro, imechukua miaka 20 kuandaa na kuratibu mpango huu,
ambao unatekelezwa sasa na hakuna uhamishaji wa nguvu unaofanywa kwa wanachi
kama inavyodaiwa, wananchi husika wameshirikishwa vya kutosha na ndio maana
wamekubali na kuamua kuhama kwa hiari wenyewe,” alisema Dkt. Ndumbaro.
Amesema Katiba ya Tanzania inasema
watu wote ni sawa na kila mtu ana haki ya kuishi popote na kuongeza kuwa
Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu wananchi wake wote bila ya kujali
rangi, kabila au dini zao.
Ameeleza kuwa wananchi wamepewa
umiliki kwa miaka kadhaa na endapo itaonekana kuna haja ya kuichaukua ardhi
hiyo anayeimiliki hulipwa fidia na kupewa ardhi katika eneo lingine na kuongeza
kuwa wananchi wanaohama kwa hiari yao kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro
wanalipwa fidia na kupatiwa nyumba za makazi, maeneo yenye huduma za kijamii na
ardhi kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Naye Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema kwamba katika wilaya ya Ngorongoro kuna
maeneo mawili ambayo yamekuwa yakizua mjadala ambayo ni eneo la hifadhi la
Ngorongoro ambalo ni urithi wa dunia na Pori Tengefu la Loliondo.
Amesema Serikali imechukua uamuzi wa
kutekeleza mpango huo kutokana na changamoto kadhaa ambazo zinatishia uhifadhi
wa eneo la Ngorongoro na kuongeza kuwa uhamaji wa hiari unaofanyika katika eneo
la Ngorongoro una lengo la kuendelea kuhifadhi eneo hilo kwa manufaa ya vizazi
vya sasa na vizazi vijavyo.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu
wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela amewahahakikishia wanadiplomasia nchini
kuwa zoezi hilo lilihusisha wananchi wa jumuiya zote waliokuwa wakiishi katika
eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kuahidi kuwa majadiliano bado yanaendelea ili
kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na uelewa wa pamoja katika suala hilo na
hivyo kufanikisha utekelezaji wa azma ya uhifadhi wa hifadhi ya Ngorongoro.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema kuwa Serikali imechukua jukumu la
kukata eneo la Loliondo SQM 4000 ambazo zina usajili na eneo la SQM 2500
likakatwa kwa ajili ya matumizi ya Wananchi.
Amesema kuwa vyombo vya habari
vimekuwa vikipotosha kuhusu eneo hilo kwa kutaka kuharibu taswira ya wawekezaji
nchini Jambo ambalo halina manufaa kwa Taifa.
” Vyombo vya habari vinapotosha
kuhusu mwekezaji aliyepo zaidi ya miaka 30 ambapo kila mwaka vitalu vya eneo
Hilo hutangazwa kisheria na kuingizwa katika minada ambapo mwekezaji huyo
huibuka mahindi na kupata eneo lake kisheria”, alisema Masanja
Mkutano huo uliohusisha viongozi
waandamizi wa serikali kutoka Wizara za mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Maliasili na Utalii, Katiba na Sheria pamoja na Wakuu wa Mikoa ya
Arusha na Tanga.
Mkutano huo ulilenga kuwafahamisha
wanadiplomasia walioko nchini juu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa
kuhama kwa hiari kunakofanywa na wananchi waliokuwa na makazi ndani ya Hifadhi
ya Ngorongoro na hivyo kuondoa sintofahamu iliyokuwepo kuwa wananchi hao
wanahamishwa kwa nguvu na serikali na hivyo kukiuka haki za binadamu.
No comments
Post a Comment