TGNP yawakutanisha wadau kupitia kijiwe cha kahawa kufuatilia bajeti kuu ya serikali 2022/2023
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) Lilian Liundi akizungumza wakati wa mjadala wa bajeti ya fedha ya Taifa kwa mwaka 2022/2023 na kueleza kuwa jitihada zaidi zinahitajika katika sekta ya kilimo ambayo ushiriki wa wanawake ni mkubwa lakini ukuaji wake umekuwa mdogo jijini Dar es Salaam.Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP,) umeendelea kuamini katika nguvu ya pamoja kwa kukutana na
wadau na wanachama wa mtandao huo na kufuatilia mgawanyo wa rasilimali kwa
kupitia bajeti kwa jicho la kijinsia.
Akizungumza wakati wa
tafakari ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia jukwaa la Kijiwe cha
Kahawa Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) Lilian Liundi amesema
kuwa jukwaa hilo litawasaidia wanajamii na wadau wa maendeleo kutambua fursa na
vipaumbele vilivyoainishwa katika bajeti pamoja na mapungufu ya kijinsia
yaliyopo katika bajeti ya mwaka husika na kutoa mapendekezo kwa watunga sera na
wahusika kuboresha zaidi ili kuwa na bajeti yenye kujenga uchumi na maendeleo endelevu
kwa taifa.
Lilian amesema kuwa, bado
kuna changamoto katika sekta za maji na kilimo katika bajeti ya mrengo wa
kijinsia na takwimu zimekuwa zikiangalia changamoto hizo kwa maeneo ya mjini
pekee na kuishauri Serikali kuu kwa kushirikiana na Serikali za mitaa kupitia Sensa
ya watu na makazi inayokwenda kufanyika ilete takwimu sahihi ya wananchi,
mahitaji yao pamoja na mgawanyo wa rasilimali kwa mrengo wa kijinsia.
Mwanamtandao wa TGNP
kutoka Kishapu, Shinyanga Bi. Fredina Said katika kueleza changamoto
wanazokumbana nazo akina Mama kujenga uchumi wa taifa kwa mrengo wa kijinsia
amesema, upatikanaji wa maji safi na salama bado imeendelea kuwa kikwazo kwa
wanawake katika kushiriki katika shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Kishapu
mkoani Shinyanga.
Amesema kuwa Kata nyingi
wilayani humo nyingi zimepitiwa na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Viktoria
ila bado hazijafikiwa na huduma hiyo kutokana na gharama ambazo wananchi
hawawezi kuzimudu.
‘’Mimi natoka Kata ya
Kiloleli kuna kata nyingi ambazo nyingine hazifanyi kazi na TGNP ila zina
changamoto kubwa ya maji kuna Kata nyingi hazijapata huduma ya maji licha ya
kupitiwa na mradi huo mkubwa…Gharama za kuunganishiwa maji zimefikia hadi
shilingi laki mbili na themanini na unit moja inalipiwa shilingi elfu mbili
kiasi ambacho mwanamke wa kijijini hawezi kukimudu’’,amesema.
Ameeleza kuwa katika
harakati za kumtua Mama ndoo kichwani Serikali kupitia bajeti lazima iangalie
namna bora ya kutatua changamoto za umbali na gharama ili wanawake ambao ndio
wazalishaji wakubwa wajikite katika shughuli za uzalishaji mali.
‘’Baadhi ya Kata
zinafuata maji kwa umbali wa Kilomita 15 na maji hayo sio salama na katika
harakati hizo hukumbana na unyanyasaji wa kijinsia, mimba za mapema na hata kwa
utoro kwa mabinti kutokana na hedhi na shuleni hakuna taulo wala maji ya
kuwasitiri’’,amesema.
Raheli Misesi kutoka
Kishapu, Shinyanga ameeleza katika sekta ya kilimo ambayo wanawake wanashiriki
kwa asilimia 80 ni vyema Serikali ikaweka mkazo na juhudi mahususi katika
kuboresha kilimo cha umwagiliaji hasa kwa wakulima wadogo vijijini.
‘’Kwa Wilaya ya Kishapu
kwa mwaka huu kumekuwa na ukame hakuna mazao kwa sasa debe moja la mahindi
linauzwa shilingi elfu kumi na nne hiki ni kiashiria kikubwa cha njaa ni vyema
Serikali ikaweka juhudi kwa kuboresha kilimo cha umwagiliaji pamoja na
teknolojia za kilimo ikiwemo matumizi ya trekta kwa wakulima wadogo na hiyo ni
pamoja na kufanya tafiti kwa mbegu na mbolea za asili ambazo zinafanya vizuri
katika ukuaji wa mazao.’’ Amesema.
Aidha amesema kuwa katika kuhakikisha bajeti inakuwa katika mrengo wa kijinsia wametembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuzungumza na wanawake na akina baba vinara kuhusu changamoto hizo na kushauri namna ya kuongeza bajeti kama TGNP wanavyofanya.
Kuhusiana na sekta ya
afya ameishukuru Serikali kwa jitihada za ujenzi wa vituo vya afya na kuiomba
kuelekeza nguvu zaidi kwa kupeleka wahudumu wa kutosha pamoja na vifaa tiba.
Jukwaa hilo
lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) limewakutanisha wananchi,
wanajamii, wachambuzi, wanasiasa na wanachama wa mtandao huo na kusikiliza kwa
pamoja uwasilishwaji wa bajeti ya Taifa na kutafakari na kujadili kwa mrengo wa
kijinsia kwa namna ambavyo bajeti kuu imeakisi kupitia sauti za wanajamii.
Mhandisi Wilhelma Malima kutoka shirika la Sanitation and Water Action (SAWA,) akichangia mada katika jukwaa la Kijiwe cha Kahawa maalumu kwa bajeti ya fedha ya mwaka 2022/2023.


.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)




.jpeg)

No comments
Post a Comment