Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt.Wilson Mahera Charles
Watanzania wametakiwa
kuwa tayari kushiriki kikamilifu zoezi la Sensa ya watu na makazi
litakayofanyika Agosti 23, 2022, nchini kote.
Wito huo umetolewa na mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt.Wilson Mahera Charles akiwa
ofisini kwake jijini Dodoma ambapo amesema kuwa zoezi la Sensa ya watu na
makazi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwani hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi
hutegemea takwimu za sensa kukadiria idadi ya wapiga kura wapya watakaoandikishwa
pamoja na waliopoteza sifa za kuandikishwa.
“Kimsingi wapiga kura au
shughuli za uchaguzi kwa ujumla zina uhusiano mkubwa na takwimu zitokanazo na
sensa, kwani katika sensa ndipo Tume inaweza kubainisha idadi ya watu
itakayowaandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura,”amesema Dkt. Mahera
na kuongeza:
“Nawahimiza watanzania
wote kujitokeza kuhesabiwa kwenye sensa ya watu na makazi mwaka huu na kila
mmoja kumhamasisha mwenzake kuhesabiwa.”
Amesema ili Tume ifanye shughuli zake vizuri ni lazima ipate
takwimu sahihi za watu, makazi na kutambua makundi maalum ambayo ni ya
wanawake, wazee, vijana na watu wenye ulemavu.
Dkt Mahera amefafanua
kuwa kutokana na sensa ya mwaka huu kufanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa
ambayo itawezesha kutambua idadi ya majengo ya umma na makazi ya watu, Tume
tutatumia takwimu hizo, kuweka vituo vya uboreshaji wa daftari la kudumu la
mpiga kura.
“Sensa ya mwaka huu
itafanyika kidigitali na itaweza kubainisha idadi ya majengo ya umma ambayo
sisi huyatumia kuweka vituo vya kujiandikisha, lakini pia itatusaidia pia
kuweka vituo hivyo kwa mujibu wa anuani za makazi ambazo pia sensa inakwenda
kuzitambua rasmi,” amesema Dkt Mahera.
Aidha amesema Tume imekua ikipanga mipango yake kwa
takwimu kuanzia ngazi ya kata lakini sasa kwa kuwa sensa inakwenda kuweka
kumbukumbu hadi ngazi ya kitongoji, itaweza kupanga mipango yake kwa urahisi
zaidi na matumizi ya teknolojia katika uchaguzi yataongezeka.
Sensa ya watu na makazi
hufanyika kila baada ya miaka 10 na mara ya mwisho Sensa hiyo ilifanyika mwaka
2012 ambapo watanzania milioni 44,929 walihesabiwa.
No comments
Post a Comment