Dkt Mabula akutana na meneja mkazi wa kampuni ya Tembo Nickel
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mhe. Dkt Angeline Mabula amekutana na kufanya mazungumzo na Meneja Mkazi wa
Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Nickel Tembo Nickel Corporation Ltd Benedict
Busunzu.
Mapema mwaka 2021 Serikali ilitia saini mkataba
na Kampuni ya LIZ Nickel ya Uingereza kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya
Nickel Kabanga mkoani Kagera, pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchenjulia
madini mbalimbali kinachojengwa Kahama, Shinyanga.
Utiaji saini wa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya LIZ Nickel kuliwezesha kuanzishwa kampuni ya pamoja inayoitwa Tembo Nickel Corporation Ltd ambayo ni kampuni ya ubia.
Akizungumza mkoani Dodoma Meneja Mkazi wa
Kampuni ya Tembo Nickel Busunzu alimueleza Waziri wa Ardhi kuwa kampuni yake
imejipanga vizuri kwa ajili ya kuanza mradi wa uchimbaji madini ya Nickel huko
Kabanga, Ngara mkoani Kagera.
Alisema, hatua ya kwanza waliyochukua ni kuwaelimisha wananchi wanaoishi eneo la mradi ili kuwajengea ufahamu kwa lengo la kuepuka migogoro wakati wa ulipaji fidia kwa wale wananchi watakaohamishwa kupisha mradi.
‘’Tumetumia muda mrefu kuwaelimisha wananchi
kabla ya kuanza uzalishaji wa Nickel hii itatusaidia kuepuka migogoro wakati wa
zoezi la ulipaji fidia kwa wale wananchi watakaohamishwa kupisha mradi’’
alisema Busunzu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Dkt Angeline Mabula alimueleza Meneja huyo kuwa, uamuzi wa kutoa elimu kwa
wananchi ni nzuri kwani utasaidia kuepuka migogoro hasa ile ya fidia kabla ya
kuanza mradi.
‘’Hatua mliyochukua ya kutoa elimu mapema ni nzuri na itasadia kuondoa migogoro wakati wa zoezi la ulipaji fidia na ni vizuri pia mkafanya utaratibu wa kuthaminisha eneo lote la mradi kama ilivyofanyika kwenye mgodi wa Nyanzaga kule Sengerema’’ alisema Dkt Mabula.
Maoteo ya awali ya uzalishaji madini ya
Nickel Kabanga wilayani Ngara mkoani Kagera utakuwa na wastani wa mauzo yenye
thamani ya dola za marekani zaidi ya milioni 664 kwa mwaka.
Katika makubaliano ya mkataba wa Mradi huo
Serikali itakuwa na umiliki usiopungua asilimia 16 ya hisa za mradi
zisizolipiwa na zisizopungua thamani, hivyo kupata gawio kwenye faida
zitakazopatikana baada ya kulipa kodi zote stahiki za serikali.
Utafiti uliofanywa na serikali ya Tanzania kuanzia mwaka 1976 -1979 ulibaini kuwepo kwa madini ya Nickel katika mwamba unaoanzia eneo la Msongati nchini Burundi hadi Kabanga ambapo kiasi kikubwa cha Nickel kinapatikana Kabanga ni ya daraja la kwanza.
No comments
Post a Comment