Waziri mkuu wa Israel kuivunja serikali na kuitisha uchaguzi mpya
Ofisi ya waziri mkuu
wa Israel Naftali Bennett imetangaza kwamba serikali ya muungano ya nchi hiyo
itavunjwa, na hivyo uchaguzi mwingine kuandaliwa.
Bennett na mshirika wake mkuu, Yair
Lapid, watalivunja bunge katika siku zijazo, ofisi ya Bennett imesema. Lapid
atahudumu kama waziri mkuu wa mpito hadi serikali mpya itakapoundwa.
Serikali ya Bennett ilikuwa dhaifu
tangu ilipoingia madarakani mwaka mmoja uliopita, muungano wa vyama vinane
tofauti unaojumuisha vyama vya mrengo wa kulia, vya kiliberali na vyama vya
Waarabu Waislamu.
Muungano huo ulianza kugawanyika baada
ya maafisa kadhaa wa chama cha Bennett kujiondoa kwenye muungano huo, wakisema
wanahisi kwamba Bennett anakubaliana maelewano mengi na washirika wake.
Uchaguzi mpya utampa fursa waziri mkuu
wa zamani wa muda mrefu Benjamin Netanyahu ya kurudi madarakani.
Netanyahu hivi sasa ni kiongozi wa
upinzani baada ya kukaa madarakani kwa miaka 12.
Siku ya Ijumaa alisema kuvunjwa kwa
bunge "itakuwa habari njema" kwa mamilioni ya Waisraeli na kutabiri
kwamba chama chake cha Likud kitaongoza serikali mpya.
Bennett aliunda serikali ya muungano wa
vyama vinane mwaka jana baada ya chaguzi nne mfululizo ambazo hazikubaini
mshindi.
Uchaguzi ujao utakuwa wa tano kwa
Israel katika kipindi cha miaka mitatu.
Waziri wa ulinzi Benny Gantz amesema
kwenye Twitter Jumatatu kwamba serikali itaendelea na shughuli zake, hata
wakati wa kipindi cha mpito.
No comments
Post a Comment