Serikali nchini Tanzania imepokea wawekezaji kutoka nchi za falme za kiarabu wenye nia ya kuwekeza kwenye kilimo cha mazao mbali mbali ikiwemo kilimo cha Parachichi katika mkoa wa Njombe.

Mbunge wa Afrika Mashariki Bi,Fancy Nkuhi akiiwakilisha nchi ya Tanzania amesema wawekezaji hao wamewasili nchini na kufika katika mkoa wa Njombe kwa nia ya kuwekeza kwenye kilimo cha Parachichi huku akibainisha kuwa ugeni huo ni matunda ya ziara ya Rais Samia aliyoifanya nchini Oman wiki mbili zilizopita.

“Nimekuja na wageni ambao wanatoka nchi za falme za kiarabu ambao wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye Sao la Parachichi kwenye mkoa wa Njombe,huu ni muendelezo wa kazi kubwa aliyoifanya Mh,Rais kwenye Ziara yake na filamu ya Royal tour”alisema Nkuhi.

Kwa mujibu wa kampuni ya BACOIN ya nchini Tanzania iliyofanikiwa kufika na wawekezaji hao mkoani Njombe imebainisha kuwa nia ya wawekezaji hao sambamba na kilimo cha Parachichi ni kufanya uwekezaji mkubwa katika  ujenzi wa kiwanda cha Nyama huku katika sekta ya utalii wakiwa na malengo ya ufugaji wa farasi.

Judica Omary ni katibu tawala wa mkoa wa Njombe kwa niaba ya mkuu wa mkoa Waziri Kindamba amesema serikali ya mkoa huo ipo tayari kuwapokea wawekezaji hao huku akihakikisha ushirikiano pamoja na upatikanaji wa ardhi.

“Nia ya uwekezaji wa hawa wageni wanahitaji ekari 100,0000 inabidi kwa mkoa wetu wa Njombe tuwapeleke katika maeneo mbali mbali,kitu kikubwa kilichonifariji ni kwa kuwa wana nia ya kuwekeza katika mazao mbali mbali”amesema Judica Omary