Anayedaiwa kutekeleza mauaji ya watu saba wa familia moja Kigoma akamatwa
Mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Peter Moris Mwandelema (33) anayedaiwa kutekeleza tukio la kuua watu saba wa familia moja mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye kijiji cha Kiganza Kigoma Vijijini mkoani Kigoma ametiwa mbaroni na jeshi la polisi mkoani humo huku ikidaiwa kuwa wivu wa mapenzi ndiyo chanzo cha mtu huyo kufanya mauaji.
Kamishna wa Operesheni na mafunzo wa jeshi la polisi, Liberatus Sabas
akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma jana alisema
kuwa mtuhumiwa ambaye fundi ujenzi na mkazi wa eneo la Mlole mjini Kigoma alikamatwa
jana mjini Kigoma.
Kamishna Sabas
alisema kuwa kulingana na mahojiano na upelelezi uliofanyika polisi
wamejiridhisha pasi na shaka kwamba mtuhumiwa huyo ndiye aliyehusika na tukio
hilo la mauaji ya watu saba akiwa peke yake bila kushirikiana na mtu yeyote
ambapo wananchi wametoa ushirikiano mkubwa wa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
Akieleza chanzo
cha tukio hilo Kamishna Sabas alisema kuwa mtuhumiwa Mwandelema alikuwa
akimtuhumu Januari Mussa mmoja wa watu waliouawa katika tukio hilo kwamba
alikuwa akitembea na mke wa mtuhumiwa ambaye kwa sasa jina lake limehifadhiwa.
Aidha Kamishna
huyo wa operesheni na mafunzo alisema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la
vitendo vya mauaji vinavyotokana na visa vya mapenzi jambo ambalo linatishia
ustawi bora wa familia.
Akizungumzia
hali hiyo Askofu wa Kanisa la EAGT kanda ya Magharibi, Omary Mlenda alisema
kuwa watu kutokuwa na hofu ya Mungu ndiyo chanzo cha mauaji yanayotokea kwa
binadamu kuuana.
Askofu Mlenda
alisema kuwa haitoshi kuingia msikitini au kanisani kuonyesha kuwa mtu huyo ni
muumini na ana hofu ya Mungu lakini matendo yake yanapaswa kuonyesha kwa
vitendo ikiwemo kuwa na uvumilivu anapopatwa na jambo.
Kamishna wa operesheni na mafunzo jeshi la polisi Liberatus Sabas akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa mtu mmoja akituhumiwa kuhusika na mauaji ya watu saba kwenye kijiji cha Kiganza Halmashauri ya wilaya Kigoma.
No comments
Post a Comment